Header Ads Widget

WIZARA YA ARDHI NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI YAIMWAGIA BILIONI 1.5 HALMASHAURI YA MJI KIBAHA.



HALMASHAURI ya Mji Kibaha imepokea kiasi cha shilingi bilioni 1.5 kutoka Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa ajili ya kupima viwanja 20,000 kwenye kata ya Pangani.


Hayo yalisemwa mjini Kibaha na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kibaha Mhandisi Mshamu Munde wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani.


Munde alisema kuwa fedha hizo ni mkopo usiokuwa na riba kwa lengo la kupima viwanja hivyo kwenye mitaa mitatu ya Kidumu, Mkombozi na Lumumba kwenye kata hiyo ya Pangani kwa kipindi cha miezi minne hadi ifikapo Aprili mwaka huu.


"Eneo hilo linakadiriwa kuwa na ukubwa wa hekta 2,963 sawa na hekari 7,407 ambalo lilikabidhiwa kwa Halmashauri ya Mji Kibaha na Wizara ya Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi," alisema Munde.


Kwa upande wake mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Kibaha Musa Ndomba alisema kuwa watakuwa makini katika utekelezaji mradi huo na mtu atakayeonekana anakwamisha hatua kali za kisheria zitachikuliwa dhidi yake.


Ndomba alisema kuwa fedha zilizokopwa ni nyingi hivyo lazima malengo yaliyowekwa yafikiwe ili mara baada ya zoezi hilo kodi ya ardhi ilipwe na kurejesha mkopo.


Naye Diwani wa kata ya Pangani Agustino Mdachi alisema kuwa kwa kushirikiana na wananchi watatekeleza mradi huo bila ya kikwazo chochote ili wananchi wapimiwe maeneo yao. 


Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI