Header Ads Widget

WATU WENYE ULEMAVU KAGERA WAIOMBA SERIKALI KUTENGA BAJETI YA FIMBO NYEUPE

WATU wenye ulemavu mkoani Kagera wameiomba serikali kupitia halmashauri zote za wilaya, kutenga bajeti kila mwaka kwa ajili ya kuwanunulia nyenzo za kujimudu kama fimbo nyeupe kwa wasioona, viti mwendo kwa wanaotambaa na shime sikio kwa viziwi, ili kuwapunguzia adha wanazokumbana nazo kutokana na kutokuwa na vifaa hivyo.



Akizungumza wakati wa mafunzo ya kutambua haki zao za kupata matibabu bure, yanayofadhiliwa na shirika la The Foundation for Civil Society, katibu wa shirikisho la vyama vya watu wenye ulemavu nchini (Shivyawata)mkoa wa Kagera, Sweetbert Mushanga alisema kuwa wengi wao hawana uwezo wa kupata fedha kwa ajili ya kununulia vifaa hivyo, kutokana na hali ngumu ya kiuchumi inayowakabili.

"Wengi wetu kutokana na ulemavu tulio nao, ambao unatufanya kushindwa kufanya kazi kikamilifu au kutofanya kazi yoyote, ni vigumu kupata fedha za kununua nyenzo za kujimudu, tunaomba angalau kila halmashauri iweke katika bajeti yake watu wenye ulemavu watano kila mwaka, wafadhiliwe vifaa hivyo" alisema Mushanga.

Aidha kuhusu suala la msamaha wa matibabu kwa kundi hilo aliiomba serikali kufikisha mwongozo wa utoaji wa huduma za afya kwa watu wenye ulemavu, katika vituo vyote vya kutolea huduma, ili waweze kutibiwa bure, kutokana na baadhi ya vituo kubainika kutokuwa na mwongozo huo.

"Lakini pia kila kata ihakikishe takwimu za watu wenye ulemavu na changamoto zinazomkabili kila mmoja wao zinapatikana kuanzia ngazi za vijiji, hii itasaidia kuwatambua na kurahisisha utoaji wa huduma kwao" alisema.

Naye Lawrian Protas ambaye ni miongoni mwa walionufaika na mafunzo hayo alisema katika masuala ya mikopo na miundombinu rafiki, wametajwa moja kwa moja, lakini kwenye Afya wanatajwa wazee, wanawake wajawazito na watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano, na watu wenye ulemavu hawatangazwi.

"Na sisi watu wenye ulemavu tunaomba tutangazwe moja kwa moja kwamba tuna msamaha wa matibabu, tuwekwe kwenye mabango kama ilivyo kwa makundi mengine, hii itatusaidia kupunguza vikwazo tunavyokumbana navyo tunapokwenda katika vituo vya kutolea huduma za Afya" alisema Protas.

Akijibu hoja hizo mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Muleba Elias Kayandabila alisema kuwa ni vigumu kuahidi kutoa huduma kwa kundi hilo kwa vitu ambavyo havikuwekwa katika bajeti, lakini akaahidi serikali kufanyia kazi baadhi ya changamoto zinazolikabili kundi hilo, kulingana na uwezo wa kifedha utaopatikana.

"Lakini sio kwamba serikali haifanyi kitu kwenu, tumekuwa tukifadhili mambo mbalimbali mfano kuwawezesha kushiriki makongamano yenu, ili mjadili kwa pamoja changamoto zinazowakabili, kwa lengo la kutafutiwa ufumbuzi" alisema.

Alisema bajeti za halmashauri hupangwa katika vikao vya maamuzi na kuwaasa kupitia vyama vyao kuwahamasisha watu wenye ulemavu kugombea nafasi mbalimbali katika chaguzi, ili wapate watu wa kuwawakilisha na kufikisha ipasavyo changamoto zinazowakabili.

"Ombi langu watu wenye ulemavu msiwe nyuma wakati wa chaguzi mbalimbali, maana ili mpate fursa ya kuingia katika vikao vya maamuzi, mfumo uliopo lazima muwe mmepita kwenye michakato ya kisiasa, mlizingatie hili kwa sasa litawasaidia kufanikisha sehemu ya mahitaji yenu" alisema.


Kuhusu matibabu bure kwa kundi hilo alisema kwa mujibu wa sera ya Afya ya mwaka 2007 pamoja na mwongozo wa msamaha, vimetoa nafasi kwa sekta ya Afya kutoa matibabu bure kwa makundi maalumu wakiwamo watu wenye ulemavu, na kwamba 

baadhi yao wamekwishanufaika na msamaha huo. 


Mwisho

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI