SHIRIKA la umeme nchini (Tanesco) linatarajia kuwafungia umeme wateja wake wapatao 2,100 kuanzia sasa hadi mwishoni mwa mwezi Machi 2022, ambao tayari wamekwishalipia gharama za kufungiwa nishati hiyo.
Meneja wa Tanesco Mkoa wa Kagera mhandisi Godlove Mathayo akizungumza baada ya uzinduzi wa jengo
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa jengo jipya la Tanesco ambalo limejengwa kwa lengo la kusogeza huduma karibu na wananchi, meneja wa shirika hilo mkoa wa Kagera mhandisi Godlove Mathayo amesema kuwa wanafanya kila jitihada ili kuhakikisha wananchi hao wanafikishiwa huduma haraka.
"Wateja hawa 2,100 wanajumuisha waliokuwa wamekwishalipia shilingi 27,000 kabla ya tamko la serikali la kupandisha gharama za kufungiwa umeme, lakini pia inajumuisha baadhi waliolipia kwa gharama mpya" amesema Mathayo.
Afisa Mkuu wa Fedha wa Tanesco Renatha Ndege akizungumza baada ya uzinduzi wa jengo
Naye Afisa Mkuu wa fedha wa Tanesco Renatha Ndege amesema wamejipanga kutoka huduma bora kwa wananchi na kupunguza malalamiko dhidi ya shirika hilo, huku akitumia fursa hiyo kuwaasa watumishi wa Tanesco kufanya kazi kwa weledi.
"Niwakumbushe watumishi wa Tanesco tupo kwa ajili ya kuhudumia wananchi wakiwamo wa Mkoa wa Kagera, tujitume katika kazi, na kama kuna mwananchi anahitaji huduma ahudumiwe kwa wakati" amesema Ndege.
Baadhi ya wakazi wa manispaa ya Bukoba ambao walikwishalipia gharama ya shilingi elfu 27 kwa ajili ya kufungiwa umeme majumbani mwao, wameliomba shirika hilo kuwafikishia huduma hiyo mapema, ili waanze kunufaika na uwepo wa nishati hiyo katika makazi yao.
"Serikali ilipotoa tamko la kupandisha gharama za umeme, lilisababisha mkanganyiko kwetu, lakini baadae walisema ambao tulikuwa tumekwishafanya malipo tutafungiwa kwa gharama hiyo, ombi letu tufungiwe kwa wakati ili malengo yetu yatimie" alisema Edger Rutechura mkazi wa Manispaa ya Bukoba.
Kwa mujibu wa meneja huyo wa Tanesco, mkoa wa Kagera kuna wateja zaidi ya 115,000 wanaohudumiwa na shirika hilo.
0 Comments