Header Ads Widget

WAKULIMA WAPEWA TAHADHARI KUELEKEA MSIMU WA MVUA

 

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Dkt. Agnes Kijazi amesema katika kipindi hichi kuelekea mvua za msimu maeneo mengi yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo mengi yanayopata mvua misimu miwili kwa mwaka.Mwandishi Fatma Ally MDTV Dar

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, amesema ongezeko la mvua linatarajiwa hususani katika kipindi cha mwezi Machi katika maeneo ya Pwani ya Kaskazini na Mwezi Aprili kwa maeneo ya Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki. 


Amesema kuwa, kwa upande wa mvua za masika zinatarajiwa kuanza mapema, kati ya wiki ya tatu na ya nne ya mwezi Februari mwaka huu na kuisha mwezi Mei mwaka huu katika maeneo mengi ya nchi.


Hata hivyo, amesema  msimu wa mvua za masika ni mahususi kwa maeneo ya Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki (Mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro), Pwani ya Kaskazini (Kaskazini mwa mkoa wa Morogoro), mikoa ya Pwani (ikijumuisha Visiwa vya Mafia), Dar es Salaam, Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba), Ukanda wa Ziwa Victora (Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara) pamoja na Kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma.


Akizungumzia Kanda ya Ziwa Victoria inayojumuisha mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Mara pamoja na Kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma (wilaya ya Kakonko na Kibondo), Dkt. Kijazi amesema mvua zinatarajiwa kuwa za wastani hadi za juu ya wastani katika maeneo mengi ya ukanda wa Ziwa Victoria pamoja na Kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma.


Amesema mvua zinatarajiwa kuanza kati ya wiki ya tatu na ya nne ya mwezi Februari mwaka huu ambapo amebainisha kuwa mvua hizo zinatarajiwa kuisha kati ya wiki ya pili ya mwezi Mei mwaka huu katika maeneo ya Kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma na Kusini wa Ziwa Victoria (Mikoa ya Geita, Mwanza na Shinyanga).


“Maeneo yaliyosalia (Kagera, Simiyu na Mara) mvua zinatarajiwa kuisha wiki ya nne ya mwezi Mei, 2022,” ameeleza Dkt. Kijazi.


Sambamba na hayo,amesema mvua hizo zitakua na manufaa katika Sekta ya Kilimo na Usalama wa Chakula kutokana na unyevunyevu wa udongo na maji ya mvua yatakayovunwa kwa ajili ya umwagiliaji vinatarajiwa kutosheleza mahitaji ya kilimo.


"Wakulima wanashauriwa kuandaa mashamba na kupanda mapema, kutumia mbinu bora na teknolojia za kuzuia maji kutuama shambani, mmomonyoko na upotevu wa rutuba na kuchagua mbegu na mazao sahihi kwa ajili ya msimu huu wa masika,” amesema Dkt. Kijazi.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI