NA WILLIUM PAUL, MOSHI.
JESHI la Polisi mkoani Kilimanjaro kwa kushirikiana na Jeshi la Uhamiaji limefanikiwa kuwakamata wahamiaji haramu 20 walioingia nchini kinyume na sheria.
Akizungumza na waandishi wa habari Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa alisema kuwa, wahamiaji wao 11 ni raia wa Ethiopia na 9 ni raia wa Somalia ambapo pia wamekamatwa Watanzania wawili waliokuwa wakiwasafirisha wahamiaji hao.
Kamanda Maigwa alisema kuwa, tukio hilo lilitokea Februari 14 mwaka huu majira ya saa moja na nusu asubuhi katika maeneo ya Ngangamfumuni kata ya Majengo wilayani Moshi askari wakiwa doria walifanikiwa kuwakamata wakiwa katika gari aina ya Toyota Landcruiser.
Alisema kuwa, gari hilo lilikuwa likiendeshwa na Mtanzania Pradius Prosper akiwa na Emman Nyembo wote wakazi wa wilaya ya Rombo ambapo katika mahojiano wahamiaji hao walidai kuwa walikuwa wanaelekea Jijini Dodoma.
Aidha alitoa wito kwa kwa Wananchi kuacha kujihusisha na vitendo vya kihalifu, kuacha tamaa za kifedha na na badala yake wajikite katika kufanya kazi na kujipatia kipato halali.
"Jeshi la polisi tumejipanga vizuri kwa doria mbalimbali masaa ishirini na nne ili kuhakikisha mkoa wa Kilimanjaro unakuwa salama pamoja na kushirikiana na Jeshi la Uhamiaji katika kuhakikisha mipaka ya nchi yetu inakuwa salama hali iliyopelekea kuwakamata wahamiaji hawa" alisema Maigwa.
Kwa upande wake, Kamanda wa Jeshi la Uhamiaji mkoa wa Kilimanjaro, Kamishna Msaidizi Edward Mwenda alisema kuwa, jeshi hilo limekuwa na ushirikiano na Jeshi la polisi ili kuhakikisha mkoa wa Kilimanjaro hauwi kimbilio la wahamiaji haramu.
Kamishna Mwenda alitumia nafasi hiyo kutoa onyo kwa Wananchi ambao sio wazalendo ambao wamekuwa wakishiriki kuwahifadhi na kuwasafirisha wahamiaji kuacha mara moja kwani watakapokamatwa watachukuliwa sheria.
Aidha Mwenda alisema kuwa, kwa mujibu wa sheria za uhamiaji inatoa adhabu mpaka miaka 20 kwa mwananchi atakayeshiriki kuwasafirisha wahamiaji haramu au kuwahifadhi pia kutaifisha chombo kilichokamatwa kikitumika kuwasafirishia wahamiaji hao pamoja na kutaifishwa kwa nyumba.
Mwisho....
0 Comments