Adeladius Makwega
DODOMA.
Nilikuwa nimelala nyumbani kwangu mara baada ya uchovu wa siku nzima ya Februari 2, 2022. Nilichukua simu yangu ya kitochi na kuwasiliana na ndugu zangu walio mbali na mimi angalau kujua kama wameshinda salama, nilifanya mazungumzo hayo kwa karibu saa nzima nikimpigia huyu na kumaliza na kumpigia mwingine.
Nilipomaliza, nilichukua chaji yangu ya simu hii angalau niweze kuiacha katika chaji ili kukicha asubuhi niweze kuwa na chaji ya kutosha. Kwani mchana wa siku hiyo nilipokea ujumbe kwenye simu yangu ya mkononi kuwa TANESCO Chamwino Ikulu inakusudia kukata umeme saa kadhaa siku inayofuata.
Nikaichukua chaji yangu na kuingiza katika soketi ya umeme na kuibonyeza kifungo cha simu hiyo na kutaka kuizima ili chaji iingie vizuri. Nikiwa na harakati hizo mara ukaingia ujumbe ukisema kuwa
“Daraja letu la Mto Ikangao limekatika hakuna kuvuka kutoka upande mmoja kwenda upande wa pili.”
Hapo zoezi langu la kuchaji simu halikuendelea tena, sikujali kuwa kesho umeme ukikatika nitaishije na simu isiyo na chaji? Je huko wote ni wazima au kuna mmoja wa jamaa zangu amepata tatizo? Akili yangu ilifikiria hilo tu.
Nilianza kumtafuta aliyenitumia ujumbe huo lakini hakupatikani, niliwapigia ndugu zangu kadhaa wa Kitongoji cha Mrundu kilichopo katika Kijiji cha Ikangao na wao hawakupatikana.
Kwa desturi ya Kata ya Ketaketa, kama mtu akiwa hapatikani kwa simu iwe Luhombero Misheni, Mrundu , Ikangao au Ketaketa, kuna kata jirani inayofahamika kama Ilonga, kata hii ndiyo iliyokuwa kata ya awali kabla ya Ketaketa. Hapo Ilonga ndipo watu wote Ketaketa walikuwa wanaitika. Ilonga kuna eneo jirani linalofahamika kama Chigandugandu.
Chigandugandu (Chiga) ni maarufu kwa mambo matatu, zamani yalikuwa mawili tu kwanza kwa Imani za kishirikina, pili kwa wachezaji wazuri wa Ngoma ya Sangura na tatu ni jipya kwani hapa ni nyumbani kwa Aishi Manula nadhani huyu ni golikipa wa Simba ya Dar es Salaam na wa timu taifa ya Tanzania.
Kwa bahati nzuri ndugu zangu hawa wa Chigandugandu wao mitandao kadhaa ya simu inapatikana, panapokuwa na shida ya dharura unampigia mtu wa Chigandugandu unamueleza ujumbe wako alafu yeye anaweza kuifunga safari iwe kwa bodaboda hadi kata ya Ketaketa iwe Misheni Luhombero, Ikangao au Ketaketa hata Mrundu na ujumbe huo utafikishwa kama ni msiba au ugonjwa.
Nilimtafuta kijana wa Chigandugandu wakala wa mitandao ya pesa za simu na yeye kumtafuta bodaboda ambaye alifunga safari hadi Ikangao kujua kilichotokea. Kijana huyu alitumia karibu saa nzima na kufuatilia kilichotokea huku akiwa huko sikuweza kupata mawasilino naye ya simu hadi aliporudi tena Chigandugandu.
Aliporudi alinitumie ujumbe huu nilipokea ujumbe. ”Mbui (mkubwa) nimesharudi naomba unipigie.”
Hiyo ilikuwa saa nne ya usiku, kijana huyu wa bodaboda aliniambia kuwa siku iliotangulia yaani Februari 1, 2022 majira ya saa moja ya jioni walisikia mlio wa kishindo katika daraja lao lilikatika, mara baada ya kukatika bila ya kujua tukio hilo gari moja ndogo ambalo lilikuwa linataka kupita bila ya kufahamu kilichotokea na giza kilikuwa kikubwa hakukuwa na mtu aliyemwembia dereva kilichojiri ndipo lilikwama kidogo kwa upande mmoja.
Mlango wa dereva ukashindwa kufunguka ndipo vijana jirani walimsaidi akatoka na kubaini kuwa alikuwa padri ambaye jina lake halikufahamika kwani alikuwa ndiyo kwanza ameripoti kuwa Paroko wa Parokia ya Ketaketa ambayo niliambiwa kuwa kwa muda mrefu ilikuwa kigango.
Ikiaminika kuwa Padri huyu alikuwa akivuka kurudi katika kituo chake kipya cha kitume ambapo asubuhi ya Februari 1, 2022 ikiaminika kuwa alipita na sasa alikuwa akirudi Ketaketa kutokea Mwaya au Mahenge.
Baada ya tukio hilo lilitafutwa trekta na kulivuta gari hiyo ndogo. Wakati wa tukio hilo ndipo na mimi nilitumiwa ujumbe ule kwa shida ya mitandao mimi niliupata usiku wa Februari, 2, 2022 saa 24 baadae.
“Yaani Padri wetu hajatuhudumia kondoo wake kwa muda mara daraja hili la Ikango linataka kutupotezea Padri wetu?” Imekuwa ikizungumzwa na wakaazi wa Ketaketa baada ya tukio hilo.
Kijana huyu aliniambia kuwa mwaka 2018 zilinyesha mvua kubwa sana na mto Ikangao ulijaa maji mengi na ukalibomoa daraja la awali ambalo lilikuwa imara sana. Likajengwa daraja shikizi la mbao na desturi madaraja kama yale ni ya kupita watu waendao kwa miguu tu hujengwa wakati wakandarasi wakiendelea na kazi na siyo daraja la kukaa miaka yote minne, maana 2018 ikapita, 2019 ikapita, 2020 ikapita, 2021 ikapita na sasa 2022 huko ni kuhatarisha uhai wa binadamu.
Kulipokucha Februari 3, 2022 ndugu yangu aliyenitumia ujumbe alifunga safari hadi Mwaya tarafani ambao hapo mitandao yote ya simu inapatikana yeye ndiyo aliniambia kila kilichotokea.
“Huku kwa sasa wakaazi hao wanalipishwa fedha kuvuka kutoka upande mmoja wa daraja kuelekea upande wa pili, wakilipa kazi ya shilingi 200 hadi 2000 kuvuka wao na vyombo vyao vya usafiri iwe ya baiskeli au pikipiki.”
Kata ya Ketaketa inapakana na Mbuga ya Selous na Mkoa wa Lindi, simulizi za wazee wanasema kuwa njia hii tangu enzi inatumika hasa na kabila la Wangindo kutoka huko Ungindoni na kwenda Upogoroni katika mambo mbalimbali ikiwamo safari za kwenda kwa kuwatembelea ndugu, kuhani misiba, kwenda kwa chifu na hata safari za kwenda kwa waganga wa kienyeji tangu enzi.
Cha kushangaza Chifu wa Wapogoro ni Mngindo anayeishi Upogoroni, kwa hiyo Wangindo ambao waliokuwa hawakai Upogoroni walikuwa wanapita njia hii kwenda kwa chifu wao. Nayasema haya kwa faida tu ya msomaji wa matini zangu tu na kuonesha umuhimu wa barabara hii na daraja hili la Ikangao kwa mkoa wa Morogoro na Lindi
Kwa kumalizia hoja ya daraja hili liwe chini TANROADS au TARURA, wananchi wa Ketaketa shida yao nikutengenezwa daraja hilo mapema ili waweze kuendelea na maisha yao kama kawaida. Kutotengeneza daraja hilo tangu libomoke awali mwaka 2018 inatosha kuwa hoja ya kulijenga kwa dharura.
Ili kuulinda uhai wa binadamu, haitopendeza tena kuandikwa au kusimuliwa habari juu ya mtu kuliwa na mamba wakati akivuka Mto Ikangao au mtu kusombwa na maji wakati akivuka Mto Ikangao maana sasa hali siyo nzuri.
Nina hakika jambo hili si la kumsumbua Mkuu wa Wilaya ya Ulanga, Mheshimiwa Ngolo Malenya au Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mheshimiwa Martine Shigela bali ni TANROADS na TARURA kwa dharura, nasema tena bali ni TANROADS na TARURA kwa dharura
Mwanakwetu kwa heshima na taadhima kwa leo naweka kalamu yangu chini.
Nakutakia siku njema.
makwadeladius@gmail.com
0717649257
0 Comments