Na,Jusline Marco;Arusha
Serikali kupitia Mamlaka ya Elimu Tanzania - TEA, imekamilisha ujenzi wa vyumba 3 vya madarasa, viti na meza 150 katika shule ya sekondari Sokon II, halmashauri ya Arusha wilaya ya Arumeru ikiwa ni uboreshaji wa miundombinu ya kufundishia na kujifunzia kwenye shule za sekondari za kata.
Mkuu wa shule sekondari Sokon II, mwalimu Prisca Mbele ameweka wazi kuwa kukamilika kwa vyumba hivyo vya madarasa kumeondoa msongamano wa wanafunzi darasani na kuwezesha shule hiyo kufikia malengo ya wastani wa wanafunzi 50, kukaa ndani ya chumba kimoja cha darasa jambo ambalo limefanikisha mazingira bora ya kujifunzia na kufundishia shuleni hapo.
Aidha Mkuu huyo wa shule amesema kuwa ujenzi wa vyumba hivyo 3 vya madarasa umegharama kiasi cha shilingi milioni 60 kutoka Mamlaka ya Elimu Tanzania, licha ya kuondoa upungufu wa vyumba hivyo vya madarasa zaidi umeondoa msongamano wa wanafunzi madarani na kuiwezesha shule hiyo kufikia mpango wa uwiano wa wanafunzi 50 kwa darasa moja.
"Ninaishukuru serikali kwa kuweka nguvu kubwa kuboresha miundombinu ya shule yetu, shule haina umri mkubwa tangu ianzishwe mwaka 2015 lakini ina miundombinu inayojitosheleza tuna madarasa ya kutosha, shule ina vyumba 27 vya madarasa , maabara 3 za masomo ya Sayansi, maabara ya somo la ICT, ofisi za walimu." amefafanua Mkuu huyo wa shule.
Naye mwalimu wa Taaluma shuleni hapo Geofrey John amesema kuwa utoshelevu wa vyumba vya madarasa shuleni hapo unawezesha walimu kuwafikia wanafunzi wote wakati wa kufundisha jambo ambalo wanaamini litaimarisha kiwango cha taaluma na kupandisha ufaulu shuleni hapo.
Vilevile ameweka wazi kuwa wameendelea kuimarika kwa kiwango cha ufaulu shuleni hapo katika mitihani ya taifa na kufikia asilimia 97.4 kwa matokeo ya kidato cha nne na asilimia 99.4 kwa matokeo ya kidato cha pili kwa mwaka 2021.
Mmoja wa wanafunzi wa kidayo cha pili shuleni hapo, Denning Innocent amethibitisha kuwa wanafunzi wote wamefurahishwa na uwepo wa madarasa ya kutosha hali itakayowapa nafasi ya kujifunza katika mazingira mazuri na kuwaongezea ari ya kujifunza.
Shule ya sekondari Sokon II iliyopo katika kata ya Kiutu ni miongoni mwa shule za kata inayokuwa kwa kasi kubwa ambayo ilianzishwa kwa nguvu za wananchi mnamo mwaka 2015 huku Serikali kwa kushirikiana na wadau wa elimu ikiweka nguvu kubwa za kuhakikisha shule hiyo inakua kwa kasi na kutimiza ndogo za wazazi walioanzisha shule hiyo.
0 Comments