Header Ads Widget

KISIASA UKRAINE ITASHINDA

 


Adeladius Makwega-DODOMA


Tangu alhamisi ya Februari 24, 2022, nimekuwa nikitumiwa ujumbe na baadhi ya rafiki zangu na wadau mbalimbali wakinishutumu kuwa mbona siandiki uchambuzi, makala au matini yoyote juu ya mgogoro baina ya Ukraine na Urusi?


Nimekuwa nikitupiwa zigo la lawama kadhaa huku na mie mwanakwetu nikizipokea kwa mikono miwili.


“Kama kweli wewe ni mchambuzi tunakuomba utuandikie habari juu ya mgogoro huo.”


Binafsi nimelitafakari jambo hili kwa kina na kusema kuwa kukaa kwangu kimya haitokuwa heshima kwao wanaotaka niandike habari juu ya mgogoro huo lakini pia haitokuwa busara kwangu mwenyewe kutolijibu jambo hilo.


Kutokuandika juu ya mgogoro huu si kwamba siutilii maanani mgogoro huo. Nautilia maanani mno, kwa hakika vita ni jambo baya, linalogharimu uhai wa binadamu wasio na hatia na vinapaswa kulaaniwa mno.


Ifahamike wazi kuwa hawa wanaopigana ni ndugu, kwa wale waliopata bahati ya kusoma USSR wakati huo wanakumbuka kuwa Ukraine na Urusi ya sasa zilikuwa chini ya shirikisho moja. 


Naomba leo hii nimkumbuke Tareq Aziz Issa (Emmanuel Yohane) ambaye alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Naibu Waziri Mkuu wa Iraki, enzi za chama Baath wakati wa Utawala wa Saddam Hussein. 


Ndugu huyu aliwahi kufanyiwa mahojiano na mtangazaji Stina Dabrowski muda mfupi kabla ya Vita vya Ghuba vya II. Ndugu Aziz alipoulizwa kama Iraki inaweza kushinda vita hivyo dhidi ya Wamarekani na washirika wake?


Alisema kuwa:


“Kunapokuwepo na mgogoro wowote wa kivita baina ya taifa kubwa dhidi ya taifa dogo, lazima taifa kubwa katika mgogoro huo kivita litashinda tu. Watafanya uharibifu na watauwa watu wengi. Lakini taifa dogo linapata nafasi ya kuonesha kuwa halikubaliani na matakwa ya taifa kubwa na matakwa hayo hayakufikiwa ndiyo maana vita vinapiganwa, kisiasa huo ni ushindi mkubwa.”


Fasili ya maneno haya ya Tareq Aziz kwa Vita vya Ukraine na Urusi ni kuwa sasa dunia inafahamu kuwa Marekani na washirika wake walifanya kosa kupambana na serikali ya chama cha Baath cha Iraki hadi kuwanyonga viongozi kadhaa waandamizi wa taifa hilo.


Ndiyo kusema Saddam Hussein alikuwa mtu salama kwa taifa hilo na dunia.


Kwa hakika hii ndiyo hali itakayotokea huko Ukraine, Urusi itashinda vita hivyo kijeshi, huku taifa la Ukraine halitokuwa salama tena, Rais Volodymyr Zelenskyy atakumbukwa kuwa alikuwa mtu sahihi kwa mustakabali wa Ukraine na Urusi.


Urusi na dunia zitabeba gharama ya vita hivyo kwa kugharamia uhalibifu wote unaoendelea na gharama yake hiyo ndiyo itakuwa funzo kwa Urusi. Wakati chuo hicho Wamarekani wameshakipitia na kufuzu katika vita vya Ghuba vya kwanza na vya pili, 


Mwanakwetu kwa leo naishi hapo huku, nikitafakari mambo ya nyumbani Tanzania hasa hasa changamoto za barabara, gharama za matibabu, changamoto za wastaafu na changamoto za elimu.


Hizi zote nitazitazama katika matini ijayo.


Nakutakia siku njema.


makwadeladius@gmail.com


0717649257

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI