Header Ads Widget

JOSEPH HAULE MSANII ANAYEYAISHI ALIYOYAIMBA I

 


Adeladius Makwega-DODOMA.


Ili maisha yaweze kwenda binadamu hawezi kufanya shughuli zake za kila siku lazima pawepo na kitu ambacho kinaweza kumliwaza iwe wakati wa kazi au hata baada ya kazi huku akiyatafakari maisha yake. 


Miongoni mwa kiliwazo nambari moja ni muziki. Ukiitazama Tanzania ya sasa na Tanzania ya mwishoni mwa miaka 1980 na 1990 hali imekuwa tofauti katika katika nyaja hiyo ya muziki.


Swali ni je huo utofauti upo wapi?


Utofauti huo unaonekana katika aina ya muziki inayosikilizwa na kupendwa hivi sasa na ile ya wakati ule.


Mathalani kijana wa kike na wakiume aliyekuwa darasa la tano, sita na saba wa miaka hiyo alikuwa akisikiliza na kuzifahamu vizuri nyimbo kadhaa za muziki wa dansi, taarabu na hata muziki kutoka Zaire (Kongo). Huku wakiziandika nyimbo hizo katika madaftari maalumu tangu mashairi na viitikio.


Hali hii ilikuwa tofauti kwa wale wanafunzi wa sekondari kwani mara baada ya kuingia sekondari vijana hao walikuwa na desturi ya kuwa madaftari yao yaliyokuwa yameandikwa nyimbo za kizungu zenye muziki wa aina mbalimbali kama vile Reggae, Blues, Rock na kadhalika huku mbinu hiyo ikitumika kujifunza Kiingereza ambayo ilikuwa ni lugha ya kujifunza na kujifunzia sekondari.


Nakumbuka nikiwa kidato cha kwanza pale Tambaza sekondari rafiki yangu mmoja anayefahamika kama Ibrahimu Liguo aliambiwa na mwalimu wa somo la Kingereza aimbe wimbo wowote wakiingereza ndugu huyu aliimba Chant down Babylon one more time wa Bob Marley. Sifahamu ndugu huyu kama hadi leo anaukumbuka wimbo huo vizuri.


Wanafunzi hao kama ndugu yangu Liguo madaftari hayo yakipambwa na picha za wanamuziki hao huku kukiwa na wasifu wa vitu wanavyovipenda na wapo walioweza kubandika picha za marafiki zao..


Kipindi hiki ndipo muziki wa kizazi kipya ulivyoweza kuibuka katika Tanzania yetu huku wanafunzi kadhaa wa sekondari wakianza kuimba nyimbo za kutunga wenyewe na wengine wakizirudia nyimbo za nje.


Mapokea ya uimbaji huo hayakuwa mazuri kwa wengi wao nikiwapo mimi ninayeandika Makala haya kwa hakika niliona hili kuwa kuimba hakukuwa na maana yoyote bali ni kupotezea muda kwa vijana wengi waliopaswa kusoma kwa bidii kwa wakati huo.


Kipindi hiki wanafunzi kadhaa walianza kuwa na tamaa ya kuwa wanamuziki na kuanza kurekodi nyimbo zao huku baadhi yao wakiwa na tuhuma ya kutumia fedha zao walizopewa na wazazi wao kama karo kutumiwa kutengeneza muziki huo.


Hoja hii na ile ya maneno yaliyokuwa yanatumiwa katika nyimbo zao kuwa meneno yasiyokuwa na tafsida ilikuwa nayo ni jiwe lililoelekea kuuzamisha muziki hii. Huku shutuma zikiwa kila upande kwa wale waliokuwa wakiufanya muziki huu wakati huo.


“Mimi na Profesa Jay tulikutana shule ya Sekondar ya Kigurunyembe mwaka 1993 hapo Morogoro, mimi nikiwa kidato cha tatu yeye akiwa kidato cha nne, kwani tabia za kupenda kuimba sote tulikuwa nazo na hazikuweza kufichwa na mazingira ya shule ya sekondari hii.” 


Maneno ya Afande Sele yanathibitisha kuwa hoja ya muziki huu ulianzia kushamiri katika shule kadhaa za sekondari za mijini.


Wazazi wengi na siye tuliokuwa tunaupinga muziki huu tulikuwa na mtazamo ule wa methali ya mshika mawili moja linamponyoka. Hatukuweka tahadhari kwa kusema kuwa mshika mawili moja linaweza kumponyoka.


Kwa hakika wapo waliofanikiwa katika muziki huo na kupoteza shule, wapo waliofanikiwa katika shule tu na wakapoteza muziki lakini pia wapo waliopoteza vyote yaani muziki na shule. 


Hapo ndipo wazazi na walezi waliokuwa wakisema mshika mawili moja litamponyoka walisema kuwa tuliwaambia vijana wetu lakini hamkusikia.Wazazi hao waliongezea methali ya mkaidi hafaidi, hadi siku ya Idi.


Joseph Haule (Profesa Jay) na Joseph Mbilinyi (Sugu). Pengine walisafiria nyota ya Yusufu (Joseph) kama majina yao yalivyo ambayekatika Biblia aliuzwa na ndugu zake kama mtumwa na akiwa utumwani akisingiziwa kesi ya kumtaka kimapenzi mke wa tajiri yake na kufungwa, lakini alishinda kizingiti hicho kwa kufanya utabiri wa ndoto ya Farao ambayo iliwashinda wengi ya masuke saba ya ngano. Hilo likamuokoa kutoka gerezani na kuwa kiongozi mkubwa huko Misri.


Peter Paul maarufu kama P Funk na sasa anaitwa Majani ni miongoni mwa watayarishaji wa muziki huo wa mwanzoni.


“Nilikutana naye mwaka 1998 na aliletwa na Profesa Ludigo na yeye ndiyo alimleta kwangu kuja kumtambulisha kwa kumwambia kuwa akitaka kufanikiwa na kuwa katika hatua ya juu ya muziki alimshauri kufanya kazi na mimi na kweli Joseph Haule alikubali na muziki wake ukaingia katika hatua nyingine ya kibiashara.”


Wakati huo vikundi kadhaa vya wanafunzi waliokuwa wakisoma shule za sekondari vilianzishwa mathalni kundi la Hard Crewz Mob


“Waanzilishi wa muziki huu akiwamo Sugu na baadaye alikuwamo yeye Profesa Jay, na Jamaa mmoja wa Hard Blasters Fanani Terry. Kuna jamaa mwingine aliyekuwa akifahamika kama Big Wile. Sisi Hard Crewz ndiyo tulikuwa tunaandaa baadhi ya  matamasha hayo, wao walikuwa wanakuja kuimba. Nawakumbuka hasa hasa Kwanza Unity, Full Crazy Flaviour, na tuliyafanya matamasha huko Crew-side-Kilimanjaro Hotel, Dar Insitute, Bilicanas na kwa kuazima vifaa kutoka kwa Josephy Kusaga.”


Anasema Modestus Makwega (Mode Fox) kutoka Hard Crewz Mob ambao wakati huo walitamba na nyimbo kama Vina Utata na Hot Portato. Akisema kuwa Kusaga aliwakodisha vyombo vya muziki Ma-DJ Charles na Bonny Lover.


Basi msomaji wangu wa matini hii nitaendelea kumtazama mwanamuziki huyu katika matini ijayo.


Nakutakia siku njema.


makwadeladius@gmail.com

0717649257

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI