Serikali imesema itaboresha mitaala ya elimu katika taasisi zake ili kukabiliana na changamoto ya uzalishaji wa ajira na ushindani wa soko la kikanda pamoja na kimataifa...............Teddy Kilanga _Arusha
Amebainisha hayo katika uzinduzi wa mfumo wa shahada ya uzamili ya usimamizi wa biashara katika uandaaji wa utekelezaji sera katika chuo cha uhasibu Arusha Mkurugenzi wa mipango wa wizara ya fedha ,Mosses Dulle amesema kupitia uboreshaji wa mitaala utaendana na mpango wa tatu wa maendeleo wa Taifa wa miaka mitano.
"Mpango huo wa tatu wa maendeleo wa Taifa wa miaka mitano unadhima ya kujenga uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu ukiwa umeainisha maeneo matano ya kipaumbele ikiwa ni pamoja na kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani na utoaji wa huduma,"amesema Dulle.
Mkurugenzi huyo amesema maeneo mengine ni pamoja na kukuza biashara na uwekezaji,kuchochea maendeleo ya watu na kuendeleza rasilimali watu hivyo ni dhahiri kuna uhitaji wa wataalamu mahiri watakaosaidia kuandaa sera madhubuti na kusaidia kutoa ushauri wa namna ya utekelezaji.
Aidha Dulle amesema mtaala huo uliozinduliwa utasaidia kuzalisha wataalamu watakaoliwezesha Taifa kufikia maono ya serikali.
Kwa upande wake kaimu Mkuu wa chuo,Dkt.Cairo Mwaitete amesema uandaaji wa sera una mchango mkubwa katika mipango na maendeleo ya Taifa ikiwa taasisi ya elimu ya IAA inatekeleza wajibu katika kutoa mafunzo kwa wanafunzi wake kwa lengo la kuandaa wataalamu watakaoleta suluhu za changamoto mbalimbali katika jamii.
"Katika kutimiza wajibu wetu tumeandaa mtaala mpya wa shahada ya uzamili ya usimamizi wa biashara katika uandaaji na utekelezaji wa sera utakaoleta tija kwa maslahi mapana ya jamii na Taifa kwa ujumla,"alisema Dkt. Mwaitete.
Kaimu mkuu huyo alisema mtaala huo utawawezesha wataalam watakaoandaliwa katika chuo hicho watahakikisha wanapata maarifa,ujuzi na mtazamo chanya katika uundaji wa sera.
Dkt. Mwaitete alisema pia mtaala huo utawawezesha wataalamu kutathmini na usimamizi katika ubunifu na ujasiriamali,uchumi na maendeleo,sera ya biashara na usimamizi wa kimkakati wa miradi,rasilimali watu pamoja na uchambuzi wa fedha za umma.
"Matarajio yetu kama chuo ni kwamba wataalam watakaosoma kozi hii watatumia dhana,nadharia na kanuni za usimamizi na utekelezaji wa sera ili kuendeleza na kupanga rasilimali na mipango ya biashara katika taasisi za umma na binafsi katika mazingira shindani,"alisema.
Sambamba na hilo alisema watatumia nadharia ,kanuni na dhana za uandaaji wa sera za maendeleo ya kiuchumi kupanga kimkakati pamoja na kutumia ujuzi wa utafiti na mbinu za takwimu za biashara katika kuunda na kuchambua sera,"alisema Kaimu mkuu wa chuo huyo.
0 Comments