Teddy Kilanga _ARUSHA
Mkurugenzi wa jiji la Arusha Dkt.John Pima amewataka vijana watakaokwenda kufanya zoezi la anwani za makazi katika kata ishirini zilizopo jijini humo kuwa waadilifu na kufata sheria na taratibu za zoezi hilo.
Alitoa maagizo hayo wakati akifungua mafunzo ya anwani za makazi kwa vijana watakaokwenda kufanya zoezi hilo katika halmashauri ya jiji la Arusha kwenye kata hizo,Dkt.Pima amesema kuwa ni vyema wakafanya kazi kwa weledi na uzalendo kwa maendeleo ya nchi yao ya Tanzania.
Aidha alisisitiza kuwa kwa kijana ambaye ni Mtanzania ndio atakaefaidika na Serikali yake,ikiwa atafanya kazi zake kwa bidii,uadilifu na kufuata sheria na taratibu za sehemu husika.
"Kama mtu nafanya kazi nzuri na kwa kujituma basi huyo ndiye atakayetumika katika kufanya kazi za serikali kama sensa,maana mtu huyo ajituma na sio mtu wa kumuelekeza wala kumsimamia,"alisema mkurugenzi Pima.
Alisema serikali inaangalia watu waojituma ili kuweza kufanya nao kazi kwani nchi hujengwa na wananchi wenyewe hivyo hawanabudi kufanya kazi kwa bidii na ufanisi wa hali ya juu ili kuweza kutekeleza zoezi hilo kwa usahihi zaidi.
Dkt Pima aliwataka vijana hao kwenda kufanya kazi vizuri kwa kuzingatia sheria na taratibu za zoezi ikiwa wapo viongozi wa kata,mitaa na waratibu wa zoezi hilo kwenda kushirikiana kwa pamoja katika kukamilisha zoezi hilo kwa weledi wa hali ya juu.
"Kazi yenu ni hiyo kutii masharti,kujituma kwa bidii kufanya kazi kwa usahihi na uangalifu mkubwa na miongozo ambayo mtapewa na maafisa wa serikali nendeni mkaisimamie hayo ndio maelekezo yangu na ndio maelekezo ya serikali,"alisema Dkt Pima.
Dkt.Pima aliwataka vijana hao kujifunza vizuri na kuelewa ili kupunguza changamoto pindi watakapokuwa katika kazi hiyo,kwani anwani ya makazi katika nchi hii ni mkombozi mkubwa na maono makubwa ya Rais wa jamuhuri ya muungano wa Tanzania ,Samia Suluhu Hassan.
Nae afisa mipango miji katika jiji hilo Ernesta Moshi ambaye pia ni msimamizi wa kata zinazowekwa anwani za makazi alisema zoezi hilo linaenda vizuri kwani wameshatoa mafunzo kwa vijana hao jinsi ya kwenda kufanya kazi ikiwa nakujipanga vyema katika kufanya zoezi hilo katika mitaa inayoendelea.
Alisema wametoa mafunzo kwa vijana hao ili kuwapa uelewa jinsi ya kwenda kufanya kazi kwa uweledi wa hali ya juu ili kupunguza changamoto zitazoweza kujitokeza katika zoezi hilo.
Moshi alisema wamepokea maelekezo ya mkurugenzi huyo hivyo wao kama wasimamizi wanaahidi kwenda kusimamia kazi hiyo kwa makini ili kupata taarifa sahihi zaidi.
Nao baadhi ya vijana katika mafunzo hayo wanakiri kupokea maelekezo ya mkurugenzi huyo ili kuweza kufanikisha kazi hiyo kwa ufanisi zaidi,kwani kazi hiyo bila kuweka maadili kazi haiwezi kwenda hivyo wanahidi kufuata sheria,kanuni na miongozo yote watakayopewa na maafisa wa serikali ili kuweza kukamilisha zoezi hilo kwa wakati na ufanisi zaidi.
Zoezi hilo lilizinduliwa na Mkuu wa mkoa wa Arusha,John Mongella mnamo februari 11,2022 na kuanza rasmi jijini Arusha katika kata tano ikiwemo Sekei,Kaloleni,Themi,Levolosi na Kati ambapo mafunzo hayo yametolewa kwa vijana watakaoendelea na zoezi hilo katika kata 20 zilizokuwa zimebaki.
0 Comments