Header Ads Widget

VIP SI SUTI NI PESA




Nilipanda bodaboda ya kunipeleka bandarini Zanzibar, niliposhuka nilimkabidhi shilingi 5000 na yeye kunirejeshea 3000, nikaondoka kuelekea bandarini, kijana huyu aliniita kwa nguvu huku akinikimbilia, akiniambia mzee, mzee, mzee ! unaenda na Helmet yangu. Hapo na mimi ndipo nilishituka kuwa nimevaa kofia hiyo. 


“Mara nyingi sana, huwa tunapoteza kofia hizo, mimi nilishapoteza kofia tano tangu Januari mwaka jana hadi sasa.” Nikamwambia pole na hata mimi nilikuwa sikumbuki kama nilikuwa nimevalia Helmet hiyo. Mara ya mwisho kuvaa Helmet ilikuwa Julai 2020 huko Mahenge Ulanga. Nilivua Helmet hii na kumpa.


Niliingia katika geti la Bandari ikiwa ni saa 9.43 Alasiri, nilionesha tiketi yangu kwa wakala wa kampuni ya Azam Marine, alipokea na kuitazama, alafu akaniambia muda bado na boti haijafika, ingia hapo ndani ukapumzike, kusubiri boti kutia nanga.


Nilitekeleza hilo na kuingia katika chumba hiki, nilipokelewa na ndugu mmoja ambaye alionekana anazungumza lugha zaidi ya nne, maana mbele yangu kulikuwa na wasafiri waliozungumza Kiarabu alijibu, Kingereza alijibu, Kiswahili alijibu na hata Kijerumani nilisikia pia alijibu.


Alinisogelea na kuitazama tiketi yangu na kuniambia kuwa mzee hapa abiria wenye tiketi kama yako huwa hawaingii, wanaoingia ni wale wa Business Class na VIP class.Kochi jirani na mimi kulikuwa na watu wakacheka. Nilitoka nje, nakusoma pale mlangoni kuna maneno gani? Hapo paliandikwa VIP LOUNGE/ CHUMBA CHA VIP. Maana ya VIP ni Very Important Person (VIP).


Nikasema moyoni kutokata kwangu tiketi ya 35,000/- au ile ya 60,000-80,000/-ndiyo nimepokonywa heshima yangu ya kuwa mtu muhimu?


Nilikumbuka mbali enzi zangu wakati najifunza habari za CCM na elimu kwa wanachama wapya, ubaya wa ubaguzi na namna wenzetu wa Afrika ya Kusini walivyokuwa wakibaguliwa kutokana na rangi zao. Wakikatazwa kuingia baadhi ya maeneo ya starehe  lakini leo hii mimi nimebaguliwa kutokana na kipato changu. Nilimkumbuka Ramadhani Nyamka aliyekuwa kiongozi wa CCM wakati huo katika mkoa wetu, Mungu amrehemu aliyetufundisha ubaya wa ubaguzi.


Nikiwa nje, nilijiuliza ilikuwaje yule jamaa wa Azam aliyeniona getini alinielekeza kwenda katika chumba hicho cha VIP au kwa kuwa nilivalia suti yangu ya rangi ya samawati? Nilijisikia mnyonge. Nikasema VIP si suti ni pesa.


Nikiwa nje, nilimuomba jamaa wa VIP nijifunze zaidi juu ya VIP LOUNGE, jamaa huyu aliniruhusu lakini akisema kuwa kwa leo nakupa ofa tu ya kupigwa na viyoyozi lakini hautopata ruhusa na kunywa chochote humu ndani.


Nikasema nashukuru kwa hisani yako hiyo, angalau na mimi nikawasimulie makabwela wenzangu habari za VIP LOUNGE, wale jamaa waliokuwa jirani na mle ndani walionicheka awali waliendelea kunicheka tena. Jamaa wa VIP Alichukua tiketi yangu na kukikata kishungi na kukichukua kipande kimoja na mimi kubaki na sehemu nyingine. 


Nikiwa mle ndani, nilibaini kweli kulikuwa na watu kutoka mataifa tofauti wakichukua vinywaji hivyo, wengine kahawa, wengine juisi, wengine soda wao na familia zao, huku mie udenda ukinitoka 


Mandhari ya VIP LOUNGE ilikuwa na makochi ya ngozi 48, meza 18 na katika samani hizo kulikuwa na sehemu za kukaa sita zilizo katika mzunguko zikijaza chumba hiki kilicho kama bweni la shule na kila sehemu hiyo ilikuwa na meza tatu. Makochi haya nane ambayo yalikuwa katika mizunguko hiyo sita, mzunguko mmoja ulikuwa na makochi ya watu watatu mawili, makochi ya watu wawili (Love seat-Bibi &Bwana) kiti kimoja na makochi ya mtu mmoja mmoja matano, jumla ya makochi yote ndiyo hayo nane.


Nilibaini kuwa katika mizunguko sita mzunguko mmoja wanaweza kukaa watu 14 jumla ya watu hao watakuwa 84 hapo ni sawa na madarasa mawili. Kwa hesabu yangu nilibaini kuwa watu waliokuwemo humo hawakuzidi 29 ambayo ni nakisi (tofauti) ya watu 55. Hata kama boti nzima waliopanda Dar es Salaam wakiingia humo kukaa na kusimama wangetosha.

Boti iliwasili na mimi kurudi zangu Dar es Salaam.


Nikiwa botini nilibaini kuwa Sultani Jamshidi Bi Abdulla yupo hai hadi sasa na ana miaka 92 akiishi huko Omani. Wakati Afro Shirazi Party ya Abeid Karume inadai uhuru walitoa fasili ya uhuru.


“Kuondoa Unyonge, Kuondoa Dhuluma, Kuondoa Shida, Kuondoa Kuogopana na Kuondoa Mengine Mengi.”


Natambua Sultani Jamshidi anayaogopa mapinduzi matukufu ya Zanzibar ambayo tuliyoyasherekea juzi, tunatakiwa kujitahidi mno kuonesha kuwa sasa tu huru, madhaifu madogo madogo yote yafanyiwe kazi.


Miaka 58 ya Mapinduzi bado tuna VIP LOUNGE/CHUMBA CHA VIP?Binafsi kwa ukweli wa Mungu nilikuwa mnyonge kutokana na tukio hilo. 


Mwisho, niwaombe ndugu zangu wa Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA) linaloongozwa na Dkt Mwanahija Ali Juma kuwa katika kila pahala palipoandikwa VIP LOUNGE tafsiri yake imeandikwa CHUMBA CHA VIP ningeomba iandikwe CHUMBA CHA WATU MUHIMU kwa kufanya hivyo tutajitambua kuwa siye siyo watu muhimu.


makwadeladius@gmail.com

0717649257

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI