Mkuu wa wilaya ya Arusha Said Mohamed Mtanda ameitaka mamlaka ya maji na usafi wa mazingira jiji la Arusha (AUWSA) kuhakikisha katika maandalizi ya mkataba wa huduma kwa mteja jambo la kwanza liwe ni kuwepo kwa mapokezi mazuri wananchi wanapofika katika ofisi zao..........NA NAMNYAK KIVUYO, ARUSHA.
Mtanda aliyasema hayo wakati akifungua kikao cha wadau katika ushirikishwaji wa kukusanya maoni juu ya maandalizi ya mkataba wa huduma kwa mteja ambapo alisema kuwa AUWSA wakitaka kutoa huduma bora ni lazima waanze na mapokezi mazuri kwa mteja.
“Muwe na ushirikiano na muda na wateja kwani mapokezi ni kitu muhimu kinachoashiria uhai wa ofisi ambapo humfanya mteja kuridhika na kuwa na uhuru wa kujieleza lakini pia muwasikilize kwa umakini na kuwahudumia,” Alisema Mtanda.
Alifafanua kuwa wanaopewa huduma ni wananchi hivyo wawape kipaumbele kwani wao ndio wadau wakubwa na ndio wanaoiweka serikali madarakani ambapo pia ameitaka mamlaka hiyo kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusiana na masuala yote ya maji safi na maji taka.
Aidha akielezea mkataba huo wa huduma kwa wateja Masoud Katiba Afisa uhusiano wa mamlaka hiyo alisema kuwa mamlaka hiyo imeandaa mkata wa huduma kwa mteja kwa madhumuni ya kuwafahamisha wateja na wakazi wa maeneo yote yanayohudumiwa na AUWSA mambo muhimu kuhusiana na huduma wanazozitoa na jinsi wanavyofanya kazi kwa kushirikiana na wateja na wadau wake kwa ujumla ambapo ni wajibu wao kutoa huduma kwa uwazi na uwajibikaji.
Alieleza kuwa mkataba huo ni mwongozo wa utendaji kazi na kilimo cha mafanikio ya huduma zinazotolewa kwani umelenga kuboresha utendaji kazi, kuongeza uwajibikaji na uwazi katika kuwahudumia wateja ambapo pia unaeleza namna ambavyo mteja atatoa mrejesho na namna ya kuwasilisha malalamiko iwapo hataridhika na huduma zinazotolewa.
“Pia mkataba unaeleza taratibu za kupata fidia pale inathibitika kuwa mteja anapata huduma chini ya viwango vinavyokubalika na mkataba huu pia utafuatiliwa ili mapungufu yanayojitokeza yatumike katika kufanya mapitio na marekebisho kwaajili ya kuongeza ufanisi wa utoaji huduma,” Alisema Katiba.
Hata hivyo baadhi wa wadau wa maji wakiwemo madiwani wa jiji la Arusha na viongozi wa serikali ngazi ya vijiji hadi wilaya waliitaka mamlaka hiyo kuboresha huduma zao hasa pale wananchi wanapotaka taarifa zitekelezwa kwa haraka pamoja kuwepo kwa uhalisia aina na muda wa malalamiko ambapo katika mkataba huo imeandikwa siku tano bila kuwa na ufafanuzi ni aina gani ya malalamiko.
0 Comments