Kampuni inayoongoza kwa utoaji wa huduma za kidigitali ya nchini, Tigo Tanzania, imedhamini Maonesho makubwa ya biashara ya mwisho wa mwaka Arusha, yanayoendelea katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, tangu Jumatatu ya tarehe 13 na yanatarajiwa kufungwa Jumapili ya tarehe 19, 2021. Ikumbukwe kuwa Maonesho haya yanayohusisha biashara mbalimbali yanalenga kutoa fursa kwa wafanyabiashara wakubwa, wa-kati na wafanyabiashara wadogo (wajasiriamali) kujitangaza na kufanya biashara hasa katika kipindi cha msimu huu wa sikukuu za mwisho wa mwaka.
Malengo mengine ya Maonesho haya ni kuwa sehemu moja ambapo wananchi wanaweza kujipatia mahitaji yao yote muhimu kimanunuzi wakati wa msimu huu wa sherehe za mwisho wa mwaka. Lakini pia Ni matarajio kuwa uwepo wa bidhaa anuai kutoka kwa washiriki kutatoa nafasi hii muhimu kwa wanunuzi kupata bidhaa zote sehemu moja. Kufanyika kwa maonesho haya kwa wiki nzima kunalenga kutoa fursa kwa wafanyabiashara kuwa na muda wa kutosha wa kufanya biashara na vilevile kwa watembeleaji kuwa na muda mrefu zaidi kufanya manunuzi.Uwanja wa Sheikh Amri Abeid pia umechaguliwa kutumika kwa sababu ya umaarufu wake, eneo uliopo na urahisi wa kufikika kwake ambapo hata wageni kutoka nje ya Jiji la Arusha wanaweza kuufikia kwa urahisi. Maonesho haya yamepangiliwa kwa mfumo wa “Mitaa” ambapo bidhaa zinazofanana hukaa eneo moja linaloitwa ‘mtaa’ na kumrahisishia mtembeleaji kujua aina za bidhaa na wapi kwa kuzipata kirahisi.
Mitaa hiyo ni Pamoja na Mtaa wa X-mas na Mwaka Mpya, Mtaa wa Shule, Mtaa wa Sola na Taa, Mtaa wa Fedha, Mtaa wa Mawasiliano na Mtaa wa Ujasiri Ni Mali.
Ushiriki wa maonesho haya unafanyika kwa njia rahisi ambapo wafanyabiashara wanafanya usajili moja kwa moja kupitia tovuti ya maonesho ya www.arushaholidayfair.com
“Kampuni ya Tigo imekuwa mstari wa mbele katika kubuni bidhaa na huduma zinazo walenga wafanyabiashara moja kwa moja kupitia huduma yetu ya Lipa Kwa Simu, tumedhamiria kuhakikisha kila mfanyabiashara atakae kuwa na banda hapa katika maonesho anatumia huduma ya Lipa Kwa Simu. Lipa kwa Simu ni huduma ya kifedha ya kidijitali inayomfanya mfanyabiashara au taasisi kupokea fedha kutoka kwa wateja wanaotumia simu za mkononi.” Aliongezea Mainoya
Gharama za viingilio katika maonesho haya ni Shs. 1,000/- kwa kulipia kupitia huduma ya Lipa Kwa Simu ya tiGO ama Tshs. 2,000/- kwa kulipia kwa pesa taslim mlangoni.
Wito unatolewa kwa wananchi wa mkoa wa Arusha na mikoa jirani kushiriki na kutembelea maonesho hili ili kujipatia bidhaa na huduma mbalimbali kipindi hiki cha msimu wa sikukuu za mwisho wa mwaka.
0 Comments