NA WILLIUM PAUL, MOSHI.
MBUNGE wa Jimbo la Moshi Vijijini mkoani Kilimanjaro Prof Patrick Ndakidemi amewahimiza wakazi wa Kibosho Kati kushiriki kikamilifu katika kuchangia miradi ya maendelo kwa kushirikiana na Serikali yao.
Prof.Ndakidemi alitoa kauli hiyo jana alipofanya ziara katika Kata ya Kibosho Kati akifuatana na Diwani wa Kata Bahati Mamboma, mwakilishi wa kamati ya Siasa CCM Wilaya, viongozi wa Chama na Serikali wa ngazi ya Kata, Vijiji na Vitongoji ambapo alikagua miradi mbalimbali ya maendeleo iliyogharimu zaidi ya milioni 300.
"Wananchi tunajukumu kubwa la kuhakikisha tunashiriki katika shughuli za maendeleo ili kuunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali yetu ya kuhakikisha inasogeza huduma karibu na wananchi wake" alisema Prof Ndakidemi.
Aidha Mbunge huyo aliwataka wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kujiunga katika vikundi ili kunufaike na mikopo inayotolewa na Halmashauri au taasisi zingine kwani bila kujiunga katika vikundi inakuwa ni vigumu kupata mikopo kutoka kwenye taasisi mbalimbali.
Mbunge huyo alihutubia mkutano wa hadhara wa kata katika kijiji cha Uri ambapo aliwasomea wananchi miradi yote iliyotekelezwa na Serikali na wadau wa maendeleo tangu aingie madarakani na kupokea changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi kutoka kwa Diwani wa Kata Bahati Mamboma na wananchi waliohudhuria.
Miradi aliyotembea ni pamoja na ile ya ujenzi wa madarasa mawili katika Shule ya Sekondari ya Mangi Sina, na vyoo katika Shule za Msingi Maseseweni na Uri ambapo miradi hii mitatu zimetumika shilingi milioni sitini na sita mia nne kutoka kwenye fedha zilizotolewa na Serikali kukabiliana na changamoto ya UVIKO 19.
Vilevile, ukaguzi ulifanyika katika mradi wa choo cha Shule ya Msingi Otaruni na Ngoroshi ambapo mfuko wa Jimbo ulitumika kugharamia baadhi ya shughuli za ujenzi.
Mbunge alijionea maendeleo ya uwekaji ya umeme katika baadhi ya Vijiji na Vitongoji vya Kata ya Kibosho Kati zikiwepo transfoma 2 mpya.
Katika ziara yake, Mbunge alishuhudia ukarabati uliofanywa na TARURA katika barabara za Otaruni - Uri, na Kwa Rafaeli hadi Mkoringa.
Pia alikagua ukarabati wa Mfereji mmoja wa asili unaofadhiliwa na mwekezaji wa shamba la maua la VASO Agroventure ambao ni muhimu sana kwa wakulima wa kahawa na migomba katika baadhi ya vijiji vya Kata ya Kibosho Kati.





0 Comments