Header Ads Widget

Kampuni ONE Acre Fund yawekeza Tsh bilioni 18 kuwezesha wakulima

  


 Waziri wa Kilimo Prof Mkenda akigawa mbolea Kwa wakulima Iringa ,mbolea iliyotolewa na kampuni ya one Acre Fund

KAMPUNI ya One Acre Fund imewekeza zaidi ya Sh Bilioni 18 zitakazowawezesha wakulima zaidi 70 wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kupata mikopo ya mbolea na mbegu bora kwa ajili ya msimu wa kilimo wa mwaka huu.

 

Mpango huo uliolezwa na Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Jennifer Lindgren kwamba “unalenga kuijenga Tanzania ambayo kila mkulima anaweza kufanikiwa” ulizinduliwa jana katika kijiji cha Ugwachanya, wilayani Iringa na Waziri wa Kilimo, Profesa Adolf Mkenda.

 

Lindgren alisema mpango huo unajumuisha tani 12,000 za mbolea na tani 300 za mbegu ambazo kwa wakulima watakaokopa watatakiwa kulipa kidogo kidogo ndani ya msimu mzima wa kilimo.

 

“Tunatamani kila mkulima  aweze kuvuna zaidi; ndio maana tuko hapa. Tunatumia nguvu nyingi kubuni njia za kuweza kufikia haya malengo, na tunajipima sio kwa faida, bali kwa matokeo wanayopata wakulima,” alisema.

 

Mkurugenzi huyo alisema kwenye ugawaji wanakodi malori ili kuwapeleka pembejo bora wakulima karibu na makazi yao lakini pia wanatoa mikopo nafuu isiyo na riba, na wafanyakazi wao hutoa mafunzo ya vitendo kwa wakulima wao  shambani katika msimu mzima.

 

pamoja na kuwekeza katika kuwakopesha wakulima mbolea na mbegu, alisema One Acre Fund imeungana na Wizara ya Kilimo kuendesha jaribio la alizeti katika wilaya ya Kilolo kwa matumaini ya kuongeza uzalishaji wake hatua inayoweza kusaidia kukabiliana na uhaba wa malighafi za kuzalishia mafuta.

 

Akilipongeza shirika hilo na kuzindua mpango huo, Profesa Mkenda alisema ili kukabiliana na upungufu wa mbolea nchini, serikali imelazimika kuingia kwenye shughuli wa uagizaji wake.

 

“Serikali pamoja na kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuondoa zabuni kwenye uagizaji wa mbolea kwa kuruhusu watu na kampuni yoyote yenye uwezo kuagiza mbolea pia imeamua kuingia kwenye uagizaji wa mbolea ili kupunguza changamoto ya upungufu wa mbolea sokoni wakati huu ambao msimu wa kilimo unakribia kuanza,” alisema.

 

Alizihimiza kampuni binafsi kuchangamkia fursa hiyo kwa kuingiza mbolea nyingi nchini hatua aliyosema itakapunguza bei ya sasa ya bidhaa hiyo ambayo ni mara mbili ya bei za mwaka jana.

 

“Kuna mfumuko wa bei ya mbolea nchini kwa sasa hali inayopelekea wakulima kushindwa kumudu gharama zake, na hali hiyo ikiendelea maana yake matumizi ya mbolea kwa msimu huu yatashuka hatua inayoweza kusababisha kilimo chetu kisiwe na tija,” alisema.

 

Awali Mkuu wa Mkoa wa Iringa Queen Sendiga alisema mkoa wake ambao ni miongoni mwa mikoa inayotegemewa kwa uzalishaji mkubwa wa mazao ya chakula, una uhitaji mkubwa wa pembejeo za kilimo ili uendelee kuzalisha chakula cha ziada.

 

Mmoja wa wakulima wa kijiji cha Ugwachanya Asifiwe Samuel aliishukuru kampuni ya One Acre Fund akisema bila wao huenda wengi wa wakulima katika mikoa hiyo wasingelima.

 

“Mkopo huu umetusaidia mno kwani wakulima wengi tulikuwa hatuwezi kumudu gharama ya sasa ya pembejeo. Mfano mbole ya DAP tuliyonunua msimu uliopita kwa Sh 50,000 sasa hivi inauzwa zaidi ya Sh 100,000. Bila mkopo huu wa One Acre Fund wengi wetu tusingeweza kumudu bei hiyo,” alisema.

 


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI