Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), mkoa wa Kilimanjaro imesema Serikali imewatengea fedha kiasi cha shilingi bilioni 15.5 kwenye sekta ya maji katika mkoa huo. mwandishi wa matukio daima Gift Mongi anaripoti kutokea Mwanga
Meneja wa RUWASA mkoa wa Kilimanjaro Mhandisi Weransari Muni, aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wilayani Mwanga wakati akizungumza kwenye kikao cha Robo ya kwanza ya mwaka 2021/2022 kikao ambacho kilikutana kwa ajili ya lengo la kujadili utekelezaji wa miradi ya maji pamoja na changamoto zilizopo ili kuboresha huduma ya upatikanaji wa maji katika mkoa huo.
Mhandisi Munis, alisema katika fedha hizo shilingi bilioni 3.5 zinatokana na fedha zilizotolewa kwa ajili ya kupambana na Uviko- 19 wakati shilingi bilioni 12 zikiwa ni fedha zilizotengwa kwenye bajeti ya mwaka 2021/2022.
Meneja huyo wa Ruwasa alisema tayari wameshatangaza zabuni 28 kwa ajili ya utekelezaji na usambazaji wa maji vijijini na kwamba kukamilika kwa miradi hiyo kutaongeza upatikanaji wa maji kwa mkoa wa Kilimanjaro.
"Kikao hiki ni cha siku mbili tutajadili changamoto zote ambazo zitalenga kwenda kuboresha huduma za maji katika mkoa wetu wa Kilimanjaro, kama ambavyo mnafahamu mkoa wa Kilimanjaro una takribani ya watu milioni 1.9 hadi sasa upatikanaji wa maji kwa maeneo ya vijijini tumefikia asilimia 83 na kwa eneo la mjini tuko katika wastani wa asilimia 91,"alisema Mhandisi Munis.
Alisema Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Moshi (MUWSA) wako katika asilimia 81 ya huduma ya utoaji maji, ambapo kwa Wilaya ya Same wako katika asilimia 42, na Wilaya ya Mwanga wako katika asilimia 62.
"Malengo ambayo tumewekewa na Serikali ifikapo mwaka 2025 huduma ya maji vijijini iwe imefikia asilimia 85, kwa mjini asilimia 95,sisi kama Sekta ya maji mkoa wa Kilimanjaro tunaimani kwamba tutafikia malengo haya ambayo yamewekwa na serikali,"alisema Mhandisi Munis.
Alisema Wilaya ya Same na Mwanga ndiyo wilaya ambazo zipo chini katika utoaji wa huduma za maji, lakini kutokana na utekelezaji wa mraji mkubwa wa maji wa Same-Mwanga-korogwe utakapokamilika miji yote hiyo ya Same na Mwanga itakuwa na uhakika wa kupata maji kwa asilimia 100.
Aidha alisema kwa upande wa maeneo ya vijijini wamebakiza asilimia mbili ya malengo tarajiwa ya serikali ya kufikisha asilimia 85.
"Serikali kwa mwaka huu wa fedha imetutengea fedha shilingi bilioni 12 kwa ajili ya kusambaza huduma za maji vijijini hadi sasa tumeshatangaza tenda za miradi hiyo zipatazo 28, zinazoenda kutekelezwa kuanzia hivi sasa,"alisema.
Munis alisema miradi ambayo itaenda kutoa huduma ya maji kwenye maeneo yote ya wilaya ambako kuna changamoto kubwa ya upungufu wa maji, lakini pia kuna uchakavu wa miundombinu ya maji ambapo kuna fedha kiasi cha shilingi bilioni 3.5 zimetengwa ambazo zitaongezwa kwenye shilingi bilioni 12 na kufikisha kiasi cha shilingi bilioni 15.5.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mwanga Abdallah Mwaipaya, alisema hali ya upatikanaji wa maji katika wilaya hiyo sio ya kuridhisha, huku akiielekeza RUWASA kuipitia upya miundombinu ya maji kwa wananchi.
"Wilaya ya Mwanga, maeneo mengi yana changamoto ya upatikanaji wa maji, na sababu kubwa inachangiwa na uchakavu wa miundombinu maji kuwa mibovu, kwani maeneo mengi maji yanapatikana lakini kutokana na uchakavu huo wa miundombinu hiyo maji hayafiki inavyostahili kwa wananchi,'alisema Mwaipaya
0 Comments