Header Ads Widget

BASHUNGWA AFUNGA SHIMIWI

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Innocent Bashungwa amezitaka Halmashauri zote nchini na Manispaa kuhakikisha viwanja vya michezo, vinakuwa moja ya vipaumbele vya miradi ya maendeleo na kutenga bajeti kila mwaka kujenga, kuboresha, na kulinda viwanja vya michezo. mwandishi wa matukio daima John Mapepele anaripoti kutokea Morogoro

Waziri Bashungwa aliyasema haya jana Novemba 2, 2021 wakati alipokuwa akifunga mashindano ya 35 ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara (SHIMIWI) mjini Morogoro ambapo alisisitiza kuwa viwanja vikiwa bora ni chanzo cha mapato kwenye Halmashauri, Manispaa na Majiji.

“Mikoa yote ya Tanzania, lazima iboreshe miundombinu ya michezo na mahitaji mengine, ili watumishi na wananchi waweze kufanya mazoezi na kushiriki kwenye mashindano mbalimbali ndani na nje ya nchi”. Alisisitiza Bashungwa

Aidha, alitoa wito kwa Wenyeviti wa Kamati za Michezo za Mikoa (Ma RAS) na Wilaya (Ma DAS) kuzingatia na kutekeleza maelekezo hayo kwa vitendo kwa kuwa Sera ya Maendeleo ya Michezo ya mwaka 1995, Sheria ya Baraza la Michezo la Taifa ya mwaka 1967, pamoja na mabadiliko yake anuai, imewapa jukumu ma RAS na ma DAS, kuhakikisha michezo inafanyika na kusimamiwa katika ngazi husika kwa ufanisi.

“Hili litafanikiwa tu ikiwa tutakuwa na miundombinu mizuri. Faida nyingine ni kwamba, tutapunguza majeraha kwa washiriki wa michezo mbalimbali wakiwa uwanjani”alisisitiza  Bashungwa

Akizungumzia kuhusu maelekezo aliyoyatoa  Dkt Phillip Isidor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakati anafungua mashindano haya Oktoba 23, 2021, kuhusu taasisi zote zinazoshiriki mashindano haya kuanza maaandalizi ya michezo hii mapema,  Bashungwa alielekeza Watendaji wa Wizara yake kusimamia na kuhakikisha kuwa tabia ya kufanya mazoezi katika maeneo ya kazi inakuwa endelevu.

Pia, kuhusu agizo la  Makamu wa Rais kwa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kufanya tathmini ya ushiriki wa kila timu na kuwasilisha taarifa za Wizara, Idara na Taasisi ambazo hazijashiriki.  Bashungwa alimhakikishia  Makamu wa Rais, kuwa tathmini hii itafanyika na taarifa itawasilishwa ofisini kwake.

Alielekeza Wizara, Mikoa na Taasisi zote za Serikali, zijipange kushiriki kwenye michezo ya SHIMIWI ijayo, kwa faida ya wafanyakazi, na ufanisi mahali pa kazi.

Bashungwa alimshukuru Rais Samia kwa kuridhia kurudisha SHIMIWI ambapo alisisitiza kuwa hatua hiyo ni nzuri, na ishara kuwa washiriki wataongezeka zaidi mwaka ujao, ili kufikia malengo ya Serikali katika kupambana na magonjwa yasiyoambukiza kama presha, kisukari na kiribatumbo.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Martine Shigela aliwashukuru waajiri kwa kuwaruhusu watumishi wao kuja kwenye mashindano hayo ambapo alisema wananchi wa mkoa wake wamenufaika kwa kiasi kikubwa.

Mwenyekiti wa SHIMIWI Taifa Daniel Mwalusamba alisema uongozi wa SHIMIWI unaiomba Serikali ushiriki wa michezo kwa watumishi wa Serikali kuwa jambo linalotekelezwa kwa mujibu wa sheria.

Mashindano ya SHIMIWI ya mwaka huu 2021 yalishirikisha Wizara 24, mikoa 11, Wakala 4 na Idara 8 za Serikali na yalihudhuriwa pia na Makatibu Wakuu kutoka Wizara ya TAMISEMI, Viwanda na Biashara na Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Mashindano haya yamefufuliwa mwaka huu kufuatia maelekezo ya  Waziri Mkuu aliyoyatoa Agosti 15, 2021 wakati akishiriki CRDB Marathon akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI