Header Ads Widget

WANANCHI WAUOMBA UONGOZI WA MKOA KUWAPATIWA VITUO VITATU VYA ELIMU YA WATU WAZIMA.

 



Na Bahati Sonda, Meatu. 


Wananchi wa kijiji cha Lukale kata ya Bukundi Wilayani Meatu Mkoani Simiyu, wameuomba uongozi wa Mkoa kuwapatia vituo vitatu vya elimu ya watu wazima kijijini hapo pamoja na walimu kutokana na kuwepo kwa wimbi kubwa la wakazi wake wasiojua kusoma wala kuandika.


Aidha kijiji hicho kipo umbali wa zaidi ya kilometa 80 kutoka makao makuu ya Wilaya hiyo huku wananchi wake wanajishughulisha na kazi za uchimbaji madini ya chumvi yanayopatikana ndani ya kijiji hicho, ufugaji pamoja na kilimo.


Wananchi hao wameyabainisha hayo jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini hapo na mbele ya  Mkuu wa mkoa wa Simiyu David Kafulila wakati alipowatembelea ili kusikiliza kero zao na kudai kuwepo kwa idadi kubwa ya wakazi wasiojua kusoma na kuandika.


Akizungumza kwa niaba ya wananchi hao, Mwenyekiti wa kitongoji cha Dumanang kilichopo kijijini hapo Girahuda Gisura, alimweleza Mkuu huyo wa Mkoa kuwa zaidi ya robo tatu ya wananchi wa kijiji hicho hawajui kusoma na kuandika.


“ Tunaomba tupatiwe walau vituo vitatu vya Memkwa kwani robo tatu ya wananchi wa kijiji cha Lukale wote hawajui kusoma na kuandika, ni kwa nini serikali isitupatie, wananchi wakanufaika angalau kujua kusoma na kuandika,” alisema Gisura.


Awali Salum Said mmoja wa wachimbaji madini ya chumvi alisema kuwa kwa muda mrefu wananchi wa kijiji hicho elimu kwao siyo kipaumbele, bali jambo muhimu ni ufugaji, uchimbaji pamoja na kilimo.


“ Wakazi wengi wa kijiji hiki ni kabila la wamangati na wataturu na kwamba wengi wao hawana elimu, hawajui kusoma na kuandika kweli kama wao walivyosema, hata sisi ambao tumekuja katika kijiji hiki tunapata shida kufanya nao kazi,” alisema Said


Kwa upande wake mtendaji wa kijiji hicho Michael Kilatu alikiri kuwepo kwa idadi kubwa ya wananchi ambao hawajui kusoma na kuandika, huku akieleza kuwa kijiji hicho kinao takribani ya wananchi 1699.


"Wananchi ambao wamesoma ni wachache sana ndani ya kijiji hiki, ila wengi hawajasoma hivyo hawajui kusoma na kuandika lakini katika suala la kuchangia shughuli za maendeleo wana mwitikio mkubwa sana hivyo kituo cha elimu ya watu wazima ni muhimu sana,” alisema Kitalu.


Hata hivyo Mkuu wa mkoa aliwashukuru wananchi kwa ombi hilo, na kumwagiza Mkurugenzi wa halmashauri hiyo pamoja na Afisa Elimu Msingi kuhakikisha wanaleta walimu na kuanzisha kituo cha elimu ya watu wazima ndani ya kijiji hicho kama hitaji la wananchi hao.


“ Nipende kuwashukuru na kuwapongeza wananchi wangu kwa ombi hilo, mmeongea jambo la muhimu sana, elimu ni haki yenu, mkurugenzi na Afisa elimu fanyeni utaratibu wa kuleta walimu na kuanzisha kituo cha Memkwa hapa mara moja,” alisema Kafulila.


Katika hatua nyingine wameiomba serikali kukamilisha ujenzi wa zahanati yao ambayo wameijenga kwa miaka 10, kwani wamekuwa wakihangaika kwa kutembea kilometa 90 kufuata huduma za Afya makao makuu ya kata.


Sambamba na Zahanati wananchi hao wameomba huduma ya Maji safi na salama kwa kuchimbiwa kisima kwani wanatoa maji mbali ambapo pia siyo safi na salama kijiji kizima ikiwa pamoja na kuomba kutengenezewa barabara.


                    Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI