Header Ads Widget

SERIKALI YAFUNGUA MILANGO ADHABU YA KIFO IJADILIWE UPYA

 


Na Arodia Peter, Dar es Salaam 


Wizara ya Sheria na Katiba imesema milango iko wazi sasa kwa wadau na jamii  kufanya mijadala kuhusu sheria inayotoa adhabu ya kifo kwa mtu anayepatikana na hatia ya mauaji na uhaini.


Msimamo huo wa Serikali umetolewa leo Oktoba 8, 2021jijini Dar es Salaam na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo,  Amon Mpanju kwenye kongamano lililoandaliwa na Jumuiya ya Umoja wa Ulaya (EU) kuhusu sheria inayoruhusu adhabu ya kifo Tanzania na Afrika Mashariki.


Kongamano hilo lilihusisha majaji wastaafu, wanasheria na  wanaharakati wa haki za binadamu wa ndani na nje ya nchi.


Mpanju alisema, ni wakati sasa kwa jamii kupitia taasisi na wadau mbalimbali kufanya mijadala na kuishauri serikali adhabu gani mbadala itumike badala ya kuendelea naya kifo ambayo inalalamikiwa kukiuka haki za binadamu.


"Sisi kama Serikali tunapongeza hatua zilizoanza kuchukuliwa na wadau wakiwamo EU kufadhili mijadala kama hii kuanza kufanyika, niombe wataalam pamoja na jamii kutazama tunaendaje kabla ya kubadili hii sheria inayotoa adhabu ya kifo kwa makosa makubwa ya mauaji na uhaini.


"Ni vizuri maamuzi ya kuondokana na adhabu ya kifo yawe ya kitaifa, zifanyike  tafiti zaidi na mijadala ishirikishe jamii kwa upana zaidi ili hatimaye tutoke na suluhisho mbadala litakalotutoa hapa tulipo.


"Samba na hilo pia tuweke nguvu ya utoaji elimu kwa jamii kuepuka kufanya matendo yanayopelekea kufikiwa kwa hizi adhabu"

alisema Mpanju.


Aidha Naibu Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Sheria na Katiba alisema ingawa baadhi ya tafiti ikiwemo Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilionyesha wananchi wanaunga mkono adhabu ya kifo iwepo nchini, lakini adhabu hiyo ni wazi inaondoa utu wa mtu na haki ya kuishi.



Naye Balozi wa EU nchini Tanzania, Manfredo Fanti alisema wameandaa kongamano hilo kuelekea Siku ya Kimataifa ya Adhabu ya kifo duniani inayoadhimishwa Oktoba 10 kila mwaka kwa lengo la kuwezesha wadau kufahamu nafasi na msimamo wa EU kuhusu adhabu ya kifo. 


Balozi Fanti alisema mpaka sasa hakuna nchi mwanachama wa EU ambayo inaendelea kutumia sheria inayoruhusu adhabu ya kifo na kwamba suala hilo wanalifanya kuwa kipaumbele chao.


Balozi huyo wa Umoja wa Ulaya aliongeza kuwa Tanzania haijatekeleza adhabu ya kifo tangu mwaka 1995 katika awamu nne tofauti za uongozi wa nchi.


Aidha Balozi Fanti alikwenda mbali zaidi kwa kunukuu kauli ya hayati Rais John Magufuli ambaye aliweka msimamo wake hadharani wa kutokusaini hati yoyote ya kifo kwa mtu yeyote na kuweka rekidi ya kipekee nchini kwa kusamehe wafungwa 62 waliokwisha kuhukumiwa kunyongwa hadi kufa.



Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI