NAIBU Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika na watu wenye Ulemavu, Ummy Nderiananga amewataka watu wenye ulemavu nchini kutumia fedha wanazokopeshwa na halmashauri kujinufaisha na kukuza kipato chao.Mwandishi William Paul anaripoti toka Same
Naibu Waziri Ummy alitoa kauli hiyo jana alipotembelea wilaya ya Same, Mwanga na Moshi mkoani Kilimanjaro na kuzungumza na watu wenye ulemavu ambapo alisema kuwa, serikali imeonyesha kuwajali watu wenye ulemavu na kupunguza masharti ya ukopaji ambapo kwa sasa anakopeshwa hata mmoja.
“Katika fedha ambapo serikali imetenga kwa kila halmashauri nchini kutoa asilimia mbili ya mapato ya ndani kwa ajili ya kuwakopesha watu wenye ulemavu tunawajibu wa kuchangamkia fedha hizo na kuzitumikia katika kukuza uchumi wetu” alisema Naibu Waziri Ummy.
Alisema kuwa, zipo baadhi ya halmashauri nchini watu wenye ulemavu wamekuwa na muamko kidogo katika ukopaji wa fedha hizo ikiwemo wilaya ya Mwanga na kutoa wito kwa maafisa ustawi wa jamii na maafisa maendeleo kuendelea kuwahamasisha kukopa.
Alisema kuwa, watu wenye ulemavu wamekuwa wakichukua mikopo ya halmashauri na kurejesha kwa wakati na kutumia nafasi hiyo kuwahamasisha kutumia fursa hiyo kukopa.
Kiongozi huyo alisema kuwa, watu wenye ulemavu wanauwezo mkubwa wa kufanya kazi ambapo alikipongeza kikundi cha watu wenye ulemavu cha Thunga group kwa jinsi walivyotumia mkopo walioupata halmashauri kuanzia duka la rejareja na wakala wa kutoa hela kwenye simu.
“Watu wenye Ulemavu hatupaswi kukata tamaa pindi tunapozarauli na wala tusibweteke wala kuvunjika moyo kwani viongozi wapo mstari wa mbele kututetea na kutuunga mkono” alisema Naibu Waziri Ummy.
Naibu Waziri Ummy alisema kuwa, Rais Samia Suluhu Hasani ametenga Bilioni 4 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni 50 ya wanafunzi wenye ulemavu ambapo kwa mkoa wa Kilimanjaro umepata mabweni mawili yatakayojengwa wilaya ya Mwanga na Moshi.
“Watu wenye ulemavu tunamshukuru sana Rais Samia kwa jinsi ambavyo anatujali na mara nyingi ameonyesha kutufariji na kujiona na sisi ni sehemu muhimu kwake na katika serikali” alisema.
Naibu Waziri huyo alitumia nafasi hiyo kuziomba halmashauri zilizopata fedha kwa ajili ya ujenzi wa mabweni kuzingatia mahitaji ya walemavu katika ujenzi wake pamoja na kusimamia fedha hizo ili thamani ya majengo iendane na thamani ya fedha.
Katika ziara hiyo, Naibu Waziri huyo alitoa vifaa saidi kwa watu wenye ulemavu katika wilaya ya Same na Moshi ambavyo ni baiskeli za mikuu mitatu 20, fimbo kwa wasioona 120 pamoja na magongo 120 ambapo ni msaaba uliotolewa na kampuni ya sigara nchini (TCC).
Akisoma taarifa ya mikopo ya watu wenye ulemavu katika wilaya ya Same, Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Anastazia Tutuba alisema kuwa katika mwaka wa fedha 2020/2021 halmashauri hiyo ilitoa mikopo ya milioni 229 katika makundi maalum ya vijina, wanawake na walemavu.
Anastazia alisema kuwa, kwa upande wa walemavu vikundi 10 vilipewa mkopo wenye thamani ya milioni 35.8 ambapo alisema mwongozo wa serikali umewawezesha watu wenye ulemavu kukopa mtu mmoja mmoja hali ambayo imesaidia kuongeza idadi ya wanaoomba mikopo.
Kwa upande wa Mkurugenzi wa Mwanga, Mwajuma Nasombe alisema kuwa, halmashauri hiyo inajumla ya watu wenye ulemavu 1341 ambapo katika mwaka wa fedha 2021/2022 halmashauri imetenga milioni 43.1 kwa ajili ya kugawa katika vikundi vya watu wenye ulemavu.
Kw upande wake, Mwenyekiti wa halmashauri ya Mwanga, Salehe Mkwizu alitumia nafasi hiyo kuiomba Serikali kujenga chuo cha ufundi kwa watu wenye ulemavu katika halmashauri hiyo ili kuwasaidia kuwajengea uwezo wa vipaji.
Mkwizu alitumia pia nafasi hiyo kusema kuwa milioni 80 za ujenzi wa bweni moja la watu wenye ulemavu fedha ambazo zimetolewa na Rais Samia zimeshafika na mwanzoni mwa mwezi Novemba ujenzi wake utaanza rasmi na kuahidi kusimamia fedha hizo kwa ukaribu.
Mwisho
0 Comments