Kamati ya Mshikamano wa Tanzania na Sahara Magharibi, inayojumuisha vijana wa
Kitanzania, inapenda kueleza azma yake ya kuendeleza fikra na misimamo dhahiri na
ya dhati ya ukombozi wa bara la Afrika, kama ilivyoasisiwa na viongozi na wazee wetu,
wakiwemo Mwalimu Nyerere na wenzake.
Nchi yetu, tangu kipindi cha kupigania uhuru na kipindi chote baada ya uhuru,
imechukua jukumu, imejivika wajibu na kuwa mstari wa mbele katika kutetea na
kusimamia azma ya ukombozi wa bara zima la Afrika.
Kama vijana wa Tanzania na Afrika, tuna kila sababu ya kihistoria na haki ya sheria na
kisiasa ya kuendeleza harakati na jitihada zote zilizoasisiwa na wazee na viongozi wetu
katika ukombozi wa bara la Afrika. Hatuna budi kuelewa kwamba ajenda ya ukombozi
wa bara la Afrika ni urithi wetu, tunapaswa kuienzi na kuiendeleza ajenda hii kwa
maendeleo ya bara letu.
Leo hii, Kamati ya Mshikamano wa Tanzania na Sahara Magharibi, tunawajibika kueleza
masikitiko yetu juu ya muenendo wa nchi ya Falme ya Morocco kuendelea kuikalia
kimabavu Jamhuri ya Kidemokrasia ya Sahara Magharibi.
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Sahara Magharibi ni nchi huru iliyopata uhuru wake kutoka
kwenye utawala dhalimu wa kikoloni wa Hispania; hata hivyo, tangu kupata uhuru wake
mwaka 1975, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Sahara Magharibi, tofauti na Tanzania na
nchi nyengine za Afrika, haijapata nafasi na wasaa wa kufurahia uhuru wake, kwani
tangu mwaka huo Morocco, ikiwa imejawa na hila, ilijitwalia mamlaka na kujimilikisha
nchi ya Sahara Magharibi; ambapo iliitangaza nchi hiyo ya Sahara Magharibi kuwa ni
sehemu ya Morocco.
Ni zaidi ya miaka 45 sasa, bado watu wa Sahara Magharibi wanadai uhuru wao kamili
kutoka kwenye makucha ya ukoloni na kukaliwa kimabavu na nchi ya Falme ya
Morocco. Sisi kama vijana wa Tanzania, tuna kila sababu ya kuungana na kushikamana
na watu wa Sahara Magharibi dhidi ya udhalimu wa Morocco.
Miaka ya karibuni, hususani tangu 2017 Morocco waliporudishwa kiholela na kupewa
uanachama katika Umoja wa Afrika ili hali nchi hiyo inakiuka misingi ya Umoja huo wa
Afrika, nchi ya Morocco wamekuwa wakieneza propaganda nchini, katika bara la Afrika
na duniani kwa ujumla dhidi ya Sahara Magharibi.
Kamati ya Mshikamano wa Tanzania na Sahara Magharibi inapinga na kukemea vitendo
vyote vya udanganyifu vinavyofanywa na vinavyolenga kuupotosha umma na vyombo
vyake kuhusu hali ya ukombozi wa nchi ya Sahara Magharibi.
Tumeshuhudia wasomi, waandishi, vyombo kadhaa vya habari na hata baadhi ya
viongozi wakiwa wahanga wa hadaa zinazoeleza kwamba eneo lote la Sahara
Magharibi ni sehemu ya Morocco. Makundi haya ya watu waliohadaika, nayo
wamegeuka na kuwa vibaraka na vinara katika kueneza na kuendeleza upotoshaji
kuhusiana na ukombozi wa Sahara Magharibi.
Jitihada hizi, zilizojaa hila, zinaendelea kwa kasi na hata tunatambua kwamba Morocco
inafanya jitihada ya kukutana na taasisi kadhaa za kiraia na viongozi wake; ambapo
inatarajia kuzitumia taasisi hizo na viongozi wa taasisi hizo katika kuwatangaza wao
kama utawala halali wa nchi ya Sahara Magharibi, kwa kuwaeleza kuwa Morocco kama
ndio suluhu ya kweli na ya kudumu katika kuisaka na kuipata amani na kuyaendea
maendeleo katika nchi ya Sahara Magharibi.
Tunaeleza kusikitishwa kwetu na makundi yote ya kijamii ambayo yamekumbwa na
upepo wa laghai za Morocco. Hivyo, kutokana na hali hii tunadhamiria kueleza kwa
makundi hayo na kwa umma wa Watanzania ya kwamba:
⦁ Sahara Magharibi ni nchi huru iliyopata uhuru mwaka 1975 na Morocco iliivamia
Sahara Magharibi na kuifanya nchi hiyo kuwa koloni lake tangu wakati huo, kwa
zaidi ya miaka 45 sasa;
⦁ Sahara Magharibi ni miongoni mwa nchi wanachama zilizounda Umoja wa Afrika
mwaka 2002 na tangu kuanza kwa Umoja wa Afrika mpaka sasa Sahara
Magharibi imekuwa ikitambulika kama nchi huru na Umoja wa Afrika (AU);
⦁ Umoja wa Mataifa unatambua eneo zima la Sahara Magharibi kama eneo la
watu wa Saharawi, watu wa Sahara Magharibi, na eneo hilo sio sehemu ya
Morocco;
⦁ Katika nyakati tofauti Mahakama ya Umoja wa Ulaya umeendelea kulitambua
eneo la Sahara Magharibi kuwa ni eneo la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Sahara
Magharibi na sio eneo la Morocco, na hivyo imebatilisha na kuzuia mikataba
mbalimbali ya kibiashara iliyoingiwa na nchi za Ulaya na Morocco iliyokuwa
ikihusianisha rasilimali za Sahara Magharibi, kwa misingi ya kwamba mikataba
yote inayohusiana na eneo na mali za Sahara Magharibi inapaswa kuingiwa na
Sahara Magharibi na sio Morocco, kwani ni nchi mbili tofauti.
Tunaeleza ya kwamba, iwapo Morocco ina dhamira ya dhati ya kuendeleza amani na
kuchangia katika maendeleo ya Sahara Magharibi na bara la Afrika, nao Morocco
hawana budi kuheshimu maamuzi ya Umoja wa Mataifa yaliyounda MINURSO na
waruhusu kufanyika kwa uchaguzi wa huru na haki utakao waruhusu watu wa Sahara
Magharibi kuamua hatma ya eneo lao – ama kujitawala au kuwa chini ya utawala wa
Morocco.
Kamati ya Mshikamano wa Tanzania na Sahara Magharibi tunatoa wito kwa taasisi za
kiraia, watetezi wa haki nchini, wasomi, waandishi na vyombo vya habari, wanasiasa,
taasisi za kiserikali na wananchi kwa ujumla, kuepuka kudanganyika na propaganda za
Morocco dhidi ya watu wa Sahara Magharibi ambapo Morocco inajaribu kuhalalisha
udhalimu wanaoufanya kwa watu hao. Hususani, tunatoa wito kwa mashirika, taasisi na
watu wote kupuuza wito na kutoshiriki semina ya kipropaganda ya Morocco inayolenga
kueleza kuhusiana na ukuu wa Morocco katika nchi ya Sahara Magharibi.
Ikiwa ni wiki ya kumuenzi Mwalimu Nyerere, Kamati ya Mshikamano wa Tanzania na
Sahara Magharibi tunaihimiza serikali kuendelea kusimamia msimamo wa nchi wa
ukombozi wa watu wa Sahara Magharibi na ukombozi wa bara zima la Afrika kama
ulivyohimizwa na kusimamiwa na Hayati Baba wa Taifa na wenzake.
Vivyo hivyo tunatoa wito kwa Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa kusimama kidete
na watu wa Sahara Magharibi na kuwanusuru na miaka mengine ya giza, kadhia,
dhoruba na tabu chini ya utawala wa kikoloni na wa kimabavu wa Morocco katika nchi
yao.
#TunasimamaNaSaharaMagharibi #TunasimamaNaAfrika





0 Comments