Mkuu wa Wilaya ya Temeke Mheshimiwa Jokate Mwegelo leo Jumamosi 30 Oktoba, 2021 amezindua Mashindano ya mchezo wa rede kwa wanawake yanayodhaminiwa na Mbunge wa Jimbo la Mbagala Mheshimiwa Abdallah Chaurembo na kujulikana kwa jina la Chaurembo Rede Cup 2021.
Uzinduzi huo uliohudhulia na Diwani wa Kata ya Chamazi Mheshimiwa John Gama, Diwani wa Kata ya Kiburugwa Mheshimiwa Fatuma Shija, viongozi wa chama na Serikali pamoja na wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam na nje ya Mkoa wa Dar es Salaam umefanyika katika Uwanja wa Shule ya Msingi Chamazi uliopo Kata ya Chamazi jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Mheshimiwa Jokate amemshukuru Mheshimiwa Chaurembo kwa kumualika kuwa Mgeni rasmi katika uzinduzi huo sambamba na kuahidi kuongeza zawadi kwa washindi.
*_"Namshukuru Mheshimiwa Chaurembo kwa kunialika kuwa Mgeni rasmi katika uzinduzi wa mashindano haya yanayohusisha wanawake wenzangu_*" alisema Jokate.
_"Baada ya kuona hamasa juu ya mchezo huu naahidi kuongeza zawadi ya 500,000/= kwa Mshindi wa kwanza, 300,000/= kwa Mshindi wa pili na 200,000/= kwa Mshindi wa tatu kwa maana hiyo ukijumlisha na zawadi za awali kwa washindi, Mshindi wa kwanza atapata 1,000,000/=, Mshindi wa Pili atapata 600,000/= na Mshindi wa Tatu atapata 400,000/=_" alisema Jokate.
Akizungumza kwa njia ya simu kutoka Dodoma Mbunge wa Jimbo la Mbagala Mheshimiwa Abdallah Chaurembo alimshukuru Mheshimiwa Jokate kwa kukubali kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa Mashindano hayo na kuahidi kuendeleza michezo ndani ya Jimbo la Mbagala.
_"Leo nilitamani kuwa na wanambagala wenzangu katika uzinduzi wa Mashindano haya kwa bahati mbaya nimepata majukumu ya Kitaifa_" alisema Chaurembo.
_"Nakushukuru Mheshimiwa Jokate kwa kukubali kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo" alisema Chaurembo.
Imetolewa na
Ofisi ya Mbunge
Jimbo la Mbagala
0 Comments