
TAASISI ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) na Shirika la Posta Tanzania (TPC) wameingia mkataba wa ushirikiano lengo ikiwa ni kutatua changamoto katika jamii kupitia wataalam wa Taasisi hizo.
Akizungumza kwenye hafla ya kusaini mkataba huo iliyofanyika jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam, Prof. Preksedis Ndomba amesema makubaliano hayo ni katika kukuza na kuendeleza uchumi wa nchi .
“Kutokana na DIT kusheheni wataalamu waliobobea katika TEHAMA, na kuzingatia kuwa Shirika la Posta limedhamiria kuboresha utendaji wake kuwa wa kidigitali wananchi wategemee kazi bora zaidi,” amesema Prof. Ndomba.
Prof. Ndomba amesema ushirikiano huo pia utaiwezesha DIT kufikia nchi nzima tofauti na sasa ambapo Taasisi hiyo ipo katika mikoa mitatu ambayo ni Dar es Salaam, Mwanza na Songwe.
Posta Masta Mkuu, Macrice Mbodo amesema makubaliano hayo ni muhimu kwa Shirika la Posta kutokana na mabadiliko makubwa yanayofanywa na Shirika hilo hivyo wanahitaji teknolojia ili waweze kufikia malengo waliyojiwekea.
“Ushirikiano huu ni wa manufaa sana kwetu kwasababu kwa kutumia wataalamu wa DIT na wa Posta tutegemee kwenda kwa kasi zaidi na kwa ubora wa hali ya juu,” alisema Mbodo.
0 Comments