Na Moses Ng’wat, Tunduma.
Wafanyabiashara wadogo wanaovuka mpaka wa Tunduma na Nakonde wamepata ahueni baada ya Tanzania na Zambia kukubaliana rasmi kuingiza bidhaa 48 katika Mpango wa Kurahisisha Biashara (Simplified Trade Regime), hatua inayolenga kuondoa masharti magumu ya kiforodha na kuchochea biashara ndogondogo mipakani.
Makubaliano hayo yamefikiwa Desemba 19, 2025, baada ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara ya Tanzania, Dkt. Hashil Twaib Abdallah, na Dkt. Simon Ng’ona, Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Viwanda ya Zambia, kuongoza zoezi la utiwaji saini wa makubaliano hayo ya utekelezaji wa STR kati ya nchi hizo mbili.
Hafla ya utiwaji saini imefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Kituo cha Pamoja cha Forodha cha mpaka (OSBP) Tunduma, na ilitanguliwa na kikao cha pamoja cha siku tatu cha wataalamu kutoka Tanzania na Zambia kilichofanyika kuanzia Desemba 17 hadi 19, 2025, kwa lengo la kuweka misingi ya kiufundi na kisheria ya utekelezaji wa mpango huo.
Akizungumza baada ya hafla hiyo, Dkt. Hashil alisema mpango wa STR ni matokeo ya mkataba wa awali uliofikiwa kati ya nchi hizo mbili, ambapo sasa jumla ya bidhaa 48 zimekubaliwa kuingia na kutoka bila wafanyabiashara wadogo kupitia taratibu ngumu za kiforodha.
Alisema utekelezaji wa mpango huo utaongeza kasi ya biashara ndogondogo, kuboresha kipato cha wananchi waishio mipakani, na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Zambia.
Aidha, alisema STR unatarajiwa kupunguza malalamiko na kero zinazowakabili wafanyabiashara wadogo, kuongeza mtiririko wa bidhaa mipakani, na kuchochea ukuaji wa uchumi kwa wananchi wa pande zote mbili.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, wakiwemo Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Prof. Godius Kahyarara, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Dkt. Maduhu Kazi, pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Zambia, Luteni Jenerali Mathiew Mkingule.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara nchini Zambia, Dkt. Ng’ona alisema makubaliano hayo yanalenga kusaidia wafanyabiashara wadogo wa Zambia na Tanzania kusafirisha bidhaa zao kupitia mipaka hiyo kwa njia halali, na kupunguza wimbi la matumizi ya njia zisizo rasmi maarufu kama “njia za panya”.
Kwa mujibu wa mkataba huo, baadhi ya bidhaa zilizojumuishwa katika mpango huo kuwa ni pamoja na nyuzi za nguo, bidhaa za dawa, sukari, nafaka, unga, sigara, bidhaa za kemikali, samani, saruji, matunda, mboga na sabuni.
Ikumbukwe kuwa mkataba wa awali wa Mpango wa Kurahisisha Biashara (STR) ulisainiwa mwaka 2017, ukiwa na bidhaa 22 pekee, hata hivyo utekelezaji wake ulikumbwa na changamoto mbalimbali kwa pande zote mbili.

.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)





0 Comments