Na,Jusline Marco:Karatu
Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro NCAA imezindua kampeni maalum ya msimu wa pili wa Merry and Wild Ngorongoro Awaits uliolenga kuwahamasisha wananchi kutembelea vivutio vilivyopo katika hifadhi ya Ngorongoro katika msimu wa sikukuu za Krismasi na mwaka mpya.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Kreta ya Empakaai iliyopo ndani ya hifadhi ya Ngorongoro Mkoani Arusha, Kamishna Msaidizi Mwandamizi Bi. Mariam Kobello ambaye pia ni Meneja Kitengo cha Huduma za Utalii na Masoko NCAA amesema katika kipindi cha sikukuu za mwisho wa mwaka NCAA Huwa na utaratibu wa kutengeneza vifurushi maalum kwa ajili ya watalii wa ndani kufika na kutembelea hifadhi ya Ngorongoro ili kujionea vivutio mbalimbali vinavyopatokana ndani ya hifadhi.
Bi. Kobello ameeleza kuwa vipo vifurushi vya aina nne ili kuwawezesha watalii kutembelea eneo la hifadhi kwa gharama nafuu ambapo amesema mkakati wa serikali ni kuhakikisha inashirikiana na sekta binafsi katika kutangaza Utalii sambamba na kuongeza idadi ya watalii ambao wanafika nchini kufanya Utalii.
Ameeleza kuwa hifadhi ya Ngorongoro Ina maeneo mengi mazuri ambayo watalii wanaweza kwenda na kufurahia mandhari mazuri yaliyopo ikiwemo Kreta ya Empakaai ambayo Ina uoto wa asilbapo amesema Kreta hiyo niya kipekee kutokana na kutoa fursa kwa mtalii kufanya Utalii wa kutembea kwa miguu ikiwa ni moja wapo ya kuimarisha afya ya mwili.
Kwa upande wake Naibu Kamishna anayeshughulikia huduma za shirika Aidan Makalla pamoja na Kuimarisha vivutio vilivyopo NCAA pia imeimarisha miundombinu ya barabara kwa ajili ya kuwezesha ufikiwaji wa vivutio kwa urahisi pamoja na huduma zote zinazotakiwa kuwepo ndani ya maeneo ya utalii.
Amewahakikishia watalii wote kuwa kutakuwepo na usalama wa kutosha katika kipindi hiki cha sikukuu ili kuhakikisha uwepo wa watalii ndani ya hifadhi.
Awali akizungumza katika uzinduzi huo mdau wa utalii kutoka kampuni ya Tanzania Smile Safaris ambaye ni Mkurugenzi wa kampuni hiyo Emmanuel Pantaleo amesema kati ya vifurushi vinne vilivyopo kipo kifurushi kinachoanzia Dar es salaam kilichopewa jina la Faru ambacho gharama yake ni shilingi 475000 huku akiainisha vifurushi vingine kama Tembo,Chui pamoja na safari ya mwaka mpya.
Ameeleza kuwa kifurushi cha Faru ambacho kinaazia jijini Dar es salaam hadi Ngorongoro kwa gharama ya 475000 na kifurushi cha Tembo ambacho kinaazia Arusha hadi Ngorongoro kinacho gharimu shilingi 450000 vinajumuisha safari ya siku mbili huku katika vifurushi vya Chui na safari ya mwaka mpya ya tarehe 1,2026 vikiwa na safari ya siku Moja kwa gharama ya shilingi 225000 ikiwa ni pamoja na gharama za kuingia hifadhini,malazi,chakula na picha.






0 Comments