Katibu tawala wilaya ya Gairo, Jeremiah Mapogo
Mwenyekiti wa Chama cha soka Mkoa wa Morogoro MWFA Beatrice Selemani
Katibu mpya wa MRFA, Alfredy Mdende maarufu kama Mteule
Na Matukio Daima Media ,Gairo,Morogoro
MKUTANO Mkuu wa Chama cha Soka Mkoa wa Morogoro (MRFA) umeidhinisha rasmi uteuzi wa Alfredy Mdende maarufu kama Mteule kuwa Mkuu mpya wa chama hicho, akichukua nafasi ya Jimmy Lengwe aliyemaliza muda wake wa karibu miaka miwili.
Uteuzi huo ulipitishwa kupitia mapendekezo ya Mwenyekiti wa MRFA, Pascal Kihanga, kwa mujibu wa katiba mpya ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) inayotoa mamlaka ya uteuzi kufanywa na Mwenyekiti badala ya uchaguzi wa moja kwa moja kama zamani kwa Baadhi ya nafasi ikiwemo hiyo.
Sambamba na Katibu mpya wa MRFA, Wajumbe hao pia wakawapitisha wajumbe wawili wapya wa kamati tendaji ya Chama jicho, mchezaji wa zamani wa Yanga Zamoyoni Mogella na Salma Mbandu.
Akizungumza katika mkutano huo uliofanyika wilayani Gairo, Kihanga alisema chama hicho kimejipanga kuimarisha ligi za ndani, programu za vijana na kutoa mafunzo kwa walimu wa soka katika ngazi zote.
“Tunataka Morogoro irejee kwenye historia yake ya kuzalisha wachezaji wakubwa nchini. Kupitia uongozi mpya, tumejipanga kuwekeza kwenye ualimu na vipaji vya vijana,” alisema Kihanga.
Katibu Mkuu mpya, Mdende, alisema atashirikiana na TFF kuhakikisha mafunzo ya ualimu wa soka yanafika ngazi za wilaya na kwamba atapigania pia kuboresha miundombinu ya michezo, ikiwemo uwanja wa Jamhuri ambao bado unahitaji maboresho makubwa sambamba na viwanja vingine vya ndani.
“Uwanja wa Jamhuri unapaswa kurudishwa kwenye hadhi yake ya kitaifa. Tutashirikiana na wadau kuhakikisha unakuwa uwanja wa mfano kwa Morogoro,” alisema Mdende.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Soka la Wanawake Mkoa wa Morogoro, Beatrice Selemani, alisisitiza umuhimu wa kuanzishwa kwa timu za wanawake zilizosajiliwa kisheria, akisema ndicho kitakuwa chanzo cha kuinua vipaji na kupata wachezaji wazuri katika ngazi mbalimbali na hata fursa ya ajira kwao.
Katibu tawala wa Wilaya ya Gairo Jeremiah Mapogo akizungumza na wajumbe hao aliahidi Serikali kuendelea kushirikiana na vyama vya soka kuhakikisha Morogoro inarejea katika hostoria Yake ya zamani ya kuwika kimichezo na kutoa wachezaji wazuri wanaoupa sifa Mkoa na Taifa Kwa ujumla.
Mwisho
0 Comments