Header Ads Widget

MKULIMA AFAFANUA SIRI YA KUVUNA KILO 3,024 ZA PAMBA KWA EKARI.


SAFARI Matonge Kusekwa, (wa pili kulia), Mkulima na mkazi wa kijiji cha Nyansalala kata ya Bukondo, wilaya ya Geita, akikabidhiwa zawadi ya kiasi cha shilingi Mil.7 baada ya kuzalisha kwa tija.


Na COSTANTINE MATHIAS, GEITA.


SAFARI Matonge Kusekwa, Mkulima na mkazi wa kijiji cha Nyansalala kata ya Bukondo, wilaya ya Geita, amejipatia umaarufu kuwa miongoni mwa wakulima wa pamba baada ya kufanikisha uvunaji wa kilo 3,024 kwa ekari moja katika msimu wa kilimo wa mwaka 2024/2025.


Hii ni rekodi mpya kwake baada ya safari ya miaka mitatu ya kuongeza uzalishaji hatua kwa hatua.


Kusekwa anasema, mwaka 2022/23 alianza kuona mwanga wa mafanikio alipovuna kilo 2,200 kwa ekari, na kufuatiwa na kilo 2,334 mwaka 2023/24. 


Kwa mwaka huu, kutokana na kutumia teknolojia za kisasa na kufuata maelekezo ya wataalamu, mavuno yake yamepanda hadi zaidi ya kilo 3,000 kwa ekari.


Kusekwa anaeleza kuwa mafanikio hayo yamechangiwa na matumizi ya vipimo sahihi vya kupanda (30/60), mbolea ya minjingu, mbolea za majani, pamoja na ujenzi wa mitaro ya kuhifadhi maji ili yasipotee shambani. 


Aidha, anasema kwa kufuata mfano wa teknolojia ya kilimo cha Brazili ambapo wakulima huvuna hadi tani 6 kwa ekari, aliamua kuwekeza zaidi katika lishe ya udongo na kumwagilia mazao.


“Ukulima wa pamba siyo wa kubahatisha, ni lazima mtu atumie mbolea zenye virutubisho, apande kwa vipimo sahihi, na zaidi ya yote asikilize ushauri wa wataalamu....Asiyefuata utaalamu huu atabaki analalamika kwa kuvuna kidogo,” anasema Kusekwa.


Anakiri kuwa msaada kutoka Serikali na wadau umechangia kuimarisha juhudi zake ambapo kituo cha Utafiki wa kIlimo Ukiriguru ilimpatia mashine ya kupanda (Rafiki Planter) ambayo imerahisisha shughuli za upandaji na kuongeza tija. 


Aidha, motisha kutoka Bodi ya Pamba Tanzania (TCB) imekuwa chachu ya kuhamasisha yeye na wakulima wenzake kuongeza bidii shambani.


“Serikali imetuheshimisha wakulima wa pamba kwa kutupatia matrekta na zana mbalimbali...hili ni jambo la kututia moyo...ni lazima tuoneshe shukrani kwa kulima kwa bidii kwa kuwa utajiri upo shambani,” anasisitiza.


Kwa mafanikio aliyoyapata, Kusekwa amepanga kulima ekari mbili katika msimu ujao, akiamini kuwa ni bora kulima eneo dogo na kulihudumia kwa uhakika badala ya kusambaza nguvu kwenye eneo kubwa lisilo na tija. 


Anasisitiza kuwa kilimo cha umwagiliaji kinaweza kuongeza mara dufu mavuno ya pamba iwapo wakulima wengi watachukua hatua hiyo.


Anatoa wito kwa wakulima wenzake kote nchini kutoshikilia kilimo cha mazoea bali kutumia utaalamu, teknolojia na zana sahihi ili kuongeza tija.


“Mimi nimeona matokeo ya kufuata maelekezo. Nawashauri wenzangu wafuate ushauri wa wataalamu wa kilimo...hapo ndipo tutajenga maisha bora kupitia zao la pamba,” anasema kwa kujiamini.


Kwa Kusekwa na wakulima wengine wa Geita, pamba siyo tu zao la biashara, bali ni nguzo ya kubadilisha maisha na kuimarisha uchumi wa familia zao.



Mwisho.





Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI