Na Fadhili Abdallah,Kigoma
WANANCHI wa mkoa Kigoma wanaelezwa kuhamasika kujitokeza kutumia majiko sanifu ikiwa ni kuunga mkono maono ya Raisi Samia Suluhu Hassan ya matumizi ya nishati safi ya kupikia katika kukabiliana na uharibifu wa mazingira.
Afisa Mahusiano wa Shirika la uzalishaji na ugavi wa umeme (TANESCO) mkoa Kigoma, Bernad Mafuru alisema hayo akizzungumza na waandishi wa habari katika mbio za mwenge wa uhuru mkoani Kigoma akieleza kuwa kwa sasa wananchi wamenza kuelewa umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Mafuru alisema wakati wa mbio za mwenge mkoani Kigoma TANESCO ilishiriki kwa mkoa mzima katika wilaya zote za mkoa huo wakiwa na banda ambalo walikuwa wakilitumia kutoa elimu, uhamasishaji lakini pia walikuwa wakiuza majiko ya umeme yanayotumia umeme kidogo.
Katika hilo Afisa Mahusiano huyo alisema alikuwa kuwa siku nane za mbio za mwenge mkoani Kigoma TANESCO Kigoma wameuza jumla ya majiko 16 ya umeme kukiwa na oda mbalimbali pia za watu wanaotaka kununua majiko hayo kuunga mkono matumizi ya nishati safi.
Kwa upande mmoja wa wateja wa matumizi ya nishati safi mkoani Kigoma,Mwenge Muyombi kutoka Shirika la Joy and The Harvest la mjini Kigoma alisema kuwa majiko hayo licha ya kutunza na kulinda mazingira pia yanatumia gharama ndogo ya umeme na kwa sasa anayo majiko matatu ambayo anatumia kwenye familia yake.
Naye Mratibu wa kitengo cha Teknolojia kutoka Shirika la viwanda vidogo (SIDO) mkoa Kigoma, Alihuru Ndedya alisema kuwa kwa sasa mwamko wa matumizi ya nishati safi na majiko sanifu na banifu imeongezeka ambapo wameanza kupata oda mbalimbali za utengenezaji wa majiko yanayotumia mkaa mbadala.
Mwisho.
0 Comments