Na Samwel Mpogole
Wizara ya Afya imeendesha mafunzo maalum ya siku mbili kwa wahariri wa vyombo vya habari nchini, yakilenga kuimarisha uelewa na kuhimiza uandishi wa habari chanya zinazohamasisha jamii kuhusu masuala ya afya.
Mafunzo hayo, yaliyofanyika katika wa Chuo cha Afya Elimu Masafa mkoani Morogoro, yamewaleta pamoja wahariri kutoka mikoa mbalimbali ili kuongeza nguvu katika kampeni za kitaifa za kuelimisha wananchi, hususan kupitia programu ya Nyumba ni Choo.
Akifunga mafunzo hayo, Mkuu wa Kitengo cha Usalama wa Chakula, Maji na Usafi wa Mazingira kutoka Wizara ya Afya, Anyitike Mwakitalima, amesema kampeni ya Nyumba ni Choo imeleta mafanikio makubwa katika kubadilisha mtazamo wa wananchi kuhusu usafi wa mazingira na afya ya jamii.
“Tumeshuhudia mabadiliko makubwa katika matumizi ya vyoo bora na usafi wa mazingira. Wizara itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali, hasa vyombo vya habari, ili kuendeleza kasi hii na kuhakikisha kila kaya inakuwa salama kiafya,” amesema Mwakitalima.
Kwa upande wake, Clara Matimo, mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, amesema wamepata ujuzi mpya wa jinsi ya kuandaa na kuwasilisha habari zinazobeba ujumbe chanya wa kiafya bila kupoteza mvuto kwa wasikilizaji na wasomaji.
“Tumejifunza namna bora ya kuunganisha takwimu, simulizi na picha halisi za jamii ili kuelimisha na kubadilisha fikra za wananchi kuhusu afya na usafi,” amesema Matimo.
Mafunzo haya yanatarajiwa kuongeza nguvu katika kupeleka ujumbe wa kiafya vijijini na mijini, huku yakilenga kuhakikisha Tanzania inafikia malengo ya afya bora kwa wote.
0 Comments