Na Matukio Daima Media
SERIKALI imempongeza Mkurugenzi wa shule ya St Anne Marie Academy ya Mbezi Kimara kwa Msuguri jijini Dar es Salaam, Dk Jasson Rweikiza kwa uwekezaji mkubwa ambao ameufanya kwenye sekta ya elimu.
Pia imeipongeza shule hiyo kwa kuendelea kufanya vizuri kitaaluma mwaka hadi mwaka katika mitihani ya kitaifa.
Pongezi hizo zilitolewa mwishoni mwa wiki na Beatrice Mbawala aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando, kwenye mahafali ya 21 ya kidato cha nne ya shule hiyo.
“Nimeambiwa hapa kwamba kuna watumishi zaidi ya 350 sasa kama shule ya St Anne Marie Academy isingekuwepo hawa wangekuwa wapi, na hawa wanandugu na jamaa wanaowategemea kwa hiyo serikali inajivunia uwekezaji huu kwasababu umepunguza tatizo la ajira nchini,” alisema
Alisema hata maendeleo ya taaluma ya shule hiyo yamekuwa yakiridhisha mwaka hadi mwaka kuanzia matokeo ya mitihani ya ngazi ya Wilaya, Mkoa na Taifa kwa kufanya vizuri kitaaluma.
“Nimejionea maonesho mbalimbali ya kitaaluma, yaani wanafunzi wanaeleza mambo mppaka unashangaa, unaweza kudhani kuwa ni wahandisi kumbe ni wanafunzi kwa kweli walimu nawapongeza mnafanya kazi kubwa sana kuwaandaa hawa wanafunzi,” alisema
“Kuna wanafunzi hapa wamezungumza lugha ya kifaransa unaweza kudhani hapa ni Paris kwa kweli walimu mnafanyakazi kubwa sana na wazazi hamuwezi kujuta kuwaleta watoto wenu St Anne Marie Academy,” alisema
Mkuu wa shule hiyo, Edrick Filemon, shule hiyo imeendelea kufanya maboresho ya miundombinu ya ubora kwa kuhakikisha inakuwa na maabara za kisasa, madarasa ya kutosha na yenye hadhi ya juu na maktaba zenye viyoyozi.
Alisema wanafunzi wa shule hiyo wamekuwa wakipewa chakula bora na cha kutosha ili wawe na nguvu na afya njema itakayowawezesha kushiriki masomo vizuri na kufanya vizuri kwenye matokeo ya kitaifa kuanzia ngazi ya kata.
Alisema shule hiyo inahuduma bora ya maji ya DAWASA na hata yakikatika wamechimba visima vikubwa vya ardhini vyenye kuhifadhi ujazo mkubwa wa maji.
Alisema kutokana na kuwepo kwa majanga ya moto kwenye maeneo mbalimbali shule hiyo imechukua tahadhari ya kuikinga na ajali zitokanazo na moto kwa kuhakikisha wanakuwa na askari wazuri wenye uwezo na mafunzo ya kuzima moto.
Alisema wanafunzi hao wanaohitimu kidato cha sita mwaka huu wameandaliwa vyema kitaaluma na asilimia kubwa wana uhakika wa kufaulu kwa kiwango cha daraja la kwanzana la pili pekee.
Alisema katika jitihada za kuhakikisha shule hiyo inaendelea kuwa juu kitaaluma, uongozi wa shule hiyo umeweka bodi ya mitihani ya shule ambayo kazi yake ni kutunga mitihani.
Alisema walimu wa shule hiyo wamebaki na kazi moja tu ya kufundisha na kazi ya kutunga mitihani imebaki kwa bodi ya mitihani ya shule na kuongeza kuwa hiyo ndiyo siri kubwa ya shule hiyo kuendelea kufanya vizuri kitaluma mwaka hadi mwaka.
0 Comments