Header Ads Widget

MGOMBEA URAIS WA CCK: “TUTAHAKIKISHA WAFANYAKAZI WANAPATA NYUMBA WAKIWA KAZINI”


Mgombea urais wa Chama Cha Kijamii (CCK), David Mwaijojele, ameahidi kuwa endapo atapewa ridhaa na Watanzania kuiongoza nchi, serikali yake itahakikisha wafanyakazi wanajengewa nyumba wakiwa bado kazini, ili kuondoa hofu ya maisha magumu baada ya kustaafu.

Akizungumza mara baada ya kuchukua fomu ya kugombea urais Akiwa na Mgombea mwenza Masoud Ali bdallah katika ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Mwaijojele amesema kuwa serikali ya CCK imejipanga kuweka mfumo wa makato maalum ya kodi kwa wafanyakazi walioko kazini, ambapo makato hayo yatatumika kuwajengea nyumba kabla hawajastaafu.

“Tumeona mara nyingi wafanyakazi waliopo kwenye ajira sasa hivi wanaogopa kustaafu kwa sababu ya mazingira wanayoishi mtu anafanya kazi miaka mingi lakini hana hata kiwanja, hana nyumba na napofikiria kuacha kazi anajiuliza ataishije.

Tunachosema sisi CCK ni kwamba, kama wananchi watatupa ridhaa ya kuongoza nchi hii, tutatengeneza mazingira mazuri ya kuwakatia kodi hizo ndogo wafanyakazi wakiwa kazini na kuzijengea nyumba zao kabla hawajastaafu,” amesema Mwaijojele.


Ameongeza kuwa lengo la mpango huo ni kuandaa mazingira salama ya ustaafu kwa watumishi wa umma na sekta binafsi, ili nafasi zao zichukuliwe na vijana, huku waliostaafu wakiendelea kuishi maisha ya heshima na hadhi.

Pamoja na hilo, Mwaijojele amesema serikali ya CCK pia ina mikakati thabiti ya kuwawezesha wananchi wa kawaida kupitia mfumo wa kuweka akiba ya kiasi kidogo cha fedha, ambapo serikali itawaunga mkono kwa kuwapatia mitaji ya kujiendeleza.

 “Hata kama mtu unaweka mia mia kwa siku, tunataka mwisho wa mwaka uweze kupata msaada kutoka serikalini hata kama una kibanda cha chumba kimoja, CCK itakusapoti ili uweze kukipanua hii ni kwa wafanyabiashara, wajasiriamali wadogo, wachimba migodi, waandishi wa habari na wananchi wote kwa ujumla,” ameeleza kwa msisitizo.

Akizungumzia mchakato wa kuchukua fomu, Mwaijojele aliishukuru Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kuratibu mchakato huo kwa weledi, akieleza kuwa tume imekuwa ikishirikiana bega kwa bega na wagombea wote tangu hatua za awali.

 “Ninawashukuru sana Mwenyekiti wa Tume, Mkurugenzi na jopo zima la Tume pamoja na wafanyakazi wote kwa kazi nzuri mnayoifanya tumekuwa tukishirikiana nanyi bega kwa bega katika kila hatua na tunathamini sana jambo hilo,” amesema.

Mwaijojele alidokeza kuwa CCK ina vipaumbele muhimu katika sekta ya kilimo cha kisasa, elimu, afya, ajira, pamoja na ustawi wa vijana na wazee.

Mwaijojele amesisitiza kuwa CCK inalenga kuleta mageuzi ya kweli kwa Watanzania wote, kwa kuhakikisha hakuna anayebaki nyuma katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

"Tunavipaumbele vingi, tuna mikakati, na tuna ilani nzuri sana ya chama. Kwa hakika ni bora kuliko zote, hata Sera ya Chma cha Mapinduzi CCM kwa sasa hatuwezi kunadi sera hadi tume itakapotuteua rasmi,” amefafanua.


 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI