Na Hamida Ramadhan, Dodoma
SHIRIKA la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) limesema linaendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali ya Tanzania kuhakikisha kunakuwa na uzalishaji bora wa mazao ya kilimo, mazingira bora ya kilimo na uwezeshaji wa wanawake kiuchumi ili kufanikisha mapinduzi ya kilimo nchini.
Kauli hiyo imetolewa Agosti 7, 2025 katika Viwanja vya Maonesho ya Kilimo na Mifugo (Nanenane) vilivyopo Nzuguni jijini Dodoma na Charles Tulai, Mwakilishi Msaidizi wa FAO, wakati wa kongamano maalum la masuala ya uwekezaji kwa wakulima na wadau wengine wa maendeleo ya sekta hiyo.
Tulai amesema mageuzi ya kilimo yana uwezo mkubwa wa kuondoa njaa na kuboresha maisha ya Watanzania, hivyo FAO itaendelea kushirikiana na Serikali katika miradi mbalimbali ya kuwawezesha wanawake na wakulima wadogo kupitia mbinu bora za uzalishaji.
Katika hatua nyingine, Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum Tanzania (TICEZA) imetangaza motisha maalum kwa Watanzania wazawa wenye nia ya kuanzisha viwanda, kwa kutoa maeneo bure ya uwekezaji kwa lengo la kuongeza ajira na kukuza pato la taifa.
Mkurugenzi Mkuu wa TICEZA, Giliard Terry, amesema hayo katika kongamano hilo, ambapo alieleza kuwa mpango huo unalenga kuchochea uwekezaji wa viwanda vya uzalishaji vitakavyomilikiwa na Watanzania, kwa ajili ya kukuza uchumi wa viwanda.
Amesema Serikali imelenga kuwa na viwanda 100 vya wazawa kwa ajili ya kuchochea ajira, hasa kwa vijana wasio na ajira rasmi, na kuwa fursa hiyo ni sehemu ya kutekeleza dira ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Terry ameongeza kuwa mnamo Agosti 12, 2025 saa 3:00 asubuhi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, anatarajiwa kuzindua rasmi huduma mpya za TICEZA, ikiwemo maeneo matano maalum ya uwekezaji.
Maeneo hayo ni pamoja na Eneo la Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, Bagamoyo (hekari 150), Dodoma (hekari 680), Buzwagi na Kwala karibu na Mlandizi (hekari 100).
Ameeleza kuwa Mtanzania yeyote mwenye nia ya kuanzisha kiwanda na ana mtaji wa kufanya hivyo, atapewa eneo bure, kwa kufuata utaratibu maalum wa mchujo utakaowekwa ili kuhakikisha wanaonufaika kweli wana uwezo wa kuwekeza na si kujilimbikizia ardhi bila kuwekeza.
Amesisitiza kuwa Serikali haitavumilia ujanja wa watu wanaotaka kumiliki maeneo kwa hila bila kuanzisha viwanda, na kwamba dhamira ni kuhakikisha Watanzania ndiyo wanufaika wakuu wa fursa za uwekezaji nchini.
0 Comments