Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Kenya Kipchumba Murkomen amewapongeza maafisa wa polisi walioweka doria Nairobi siku ya Jumatatu kwa jukumu lao la kudumisha utulivu na kupunguza ghasia wakati wa maandamano ya Saba Saba.
Katika taarifa iliyotolewa baada ya kuzuru sehemu za mji mkuu, Murkomen aliwasifu maafisa wa polisi kwa kile alichokiita "kujitolea kwao kulinda maisha na mali" wakati wa maandamano, yaliyoadhimisha miaka 35 ya vuguvugu la kuunga mkono demokrasia la Saba Saba nchini Kenya.
Alielezea utendaji wao kama "wa kupongezwa na muhimu kwa usalama wa umma."
"Saba Saba inaadhimisha siku ya mabadiliko katika safari ya nchi yetu kuelekea demokrasia ya vyama vingi, utaratibu na utawala bora. Wakenya wana haki ya kuadhimisha siku hiyo kwa amani na adabu," Murkomen alisema.
"Kwa bahati mbaya, maandamano ya amani hivi karibuni yameingiliwa na wahalifu ili kusababisha fujo na uharibifu."
Alibainisha kuwa kutokana na kuongezeka kwa ulinzi nchini kote, matukio ya ghasia, uporaji na uharibifu "yalipungua kwa kiasi kikubwa" ikilinganishwa na maandamano ya awali, hasa yale ya Juni 25, ambayo yalishuhudia uharibifu na makabiliano makubwa.
Murkomen amesema watu waliohusika na usumbufu wa Jumatatu watachunguzwa na kufunguliwa mashtaka, kama ilivyofanywa kwa wale waliohusika katika maandamano ya ghasia hapo awali.
0 Comments