NA CECILIA PIUS MATUKIO DAIMA MEDIA
ALIYEKUWA diwani wa kata ya Mkimbizi Halmashauri ya Manispaa ya Iringa Eliud Mvella amesema mchakato wa ujenzi wa barabara ya lami kilomita 5.1 itakayounganisha kata ya Mkimbizi na Mtwivila umefikia hatua nzuri na tayari mkandarasi amekwisha wasili kukabidhiwa eneo la kuanza ujenzi huo .
Kuwa ujenzi huo utatoa fursa kuwa kwa wananchi wa kata ya Mkimbizi na Mtwivila ambao wanasifa ya kufanya kazi mbali mbali katika mradi huo pia wale wenye biashara mbali mbali kwani wafanyakazi wa mradi huo watahitaji huduma kutoka kwao.
Akizungumza katika kipindi cha Tanzania ya Leo kilichorushwa na Matukio Daima Tv Mvella alisema kuwa ujenzi wa barabara hiyo ni matokeo mazuri ya kazi zinazofanywa na serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan na wao katika wasaidizi wake ngazi ya kata ya aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo Jesca Msambatavangu kuwa msimamizi ngazi ya jimbo miradi hiyo imekuwa kielelezo kizuri .
" Tunamshukuru Sana mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri kwani ujenzi wa barabara hii utakuwa mkombozi mkubwa wa maendeleo na uchumi wa wananchi wa kata ya Mkimbizi pia Manispaa ya Iringa ambao watanufaika na barabara hiyo "
Alisema kuwa barabara ya Mkimbizi -Mtwivila imekuwa kero kubwa kwa wananchi na watumiaji wa barabara hiyo kutokana na ubovu uliokithiri hasa wakati wa masika kutokana na barabara hiyo kutopitika kwa urahisi .
Hivyo alisema hatua ya ujenzi huo kuanza utasaidia kuondokana na changamoto hiyo ya ubovu wa miundo mbinu kwani ujenzi huo utachagiza ukuaji wa uchumi kwa wananchi wa eneo hilo.
Mvella alisema tayari mkataba wa ujenzi wa barabara hiyo umekwisha sainiwa toka Juni 25 na mkandarasi amefika kuoneshwa eneo la mradi toka Julai 15 mwaka huu na kuwa wakati wowote kazi itaanza baada ya mkandarasi huyo kulipwa fedha anzio za kazi hiyo .
Hata hivyo aliwataka wananchi wa Mkimbizi kuendelea kuwa na matumaini na serikali ya chama cha mapinduzi (CCM) kwani ipo kwa ajili ya kuwatumikia na kutatua changamoto mbali mbali kama ilivyofanya katika sekta ya elimu na afya .
0 Comments