Header Ads Widget

TAKUKURU YAKEMEA RUSHWA YA NGONO VYUONI


Na Thobias Mwanakatwe,SINGIDA

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Sigida, imewataka wananchi  na wanafunzi waliopo katika vyuo kutoa taarifa wanapofanyiwa vitendo vya rushwa ya ngono ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa kwa wahusika.

Mkuu wa Dawati la Elimu kwa Umma TAKUKURU Mkoa wa Singida, Benjamin Masyaga, amesema hayo leo (Julai 28, 2025) wakati wa uzinduzi wa Dawati la Jinsia katika Chuo cha Ufundi Stadi na Marekebisho kwa watu wenye ulemavu Sabasaba kilichopo Manispaa ya Singida.

“Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa sura ya 329 marejeo ya mwaka 2022 imetamka kosa hili chini ya kifungu cha 25 ambapo kwa tafsiri isiyo rasmi inaeleza mtu yeyote ambaye kwa kutumia nafasi yake au mamlaka yake katika kutekeleza majukumu yake anadai au analazimisha upendeleo wa kingono au upendeleo mwigine wowote kwa kigezo cha kutoa ajira, kupandishwa cheo, kutoa haki au upendeleo wowote unaotambulika kisheria atakuwa ametenda kosa,”amesema Masyaga.

Amesema rushwa ya ngono imekuwa na madhara mengi ikiwapo mimba za utotoni zisizotarajiwa, kupoteza nguvu kazi ya taifa, kusababisha vifo kwa wanaofanyiwa vitendo hivyo,inadhalilisha utu na heshima, inakiuka haki za binadamu,inaongeza maambukizi ya magonjwa ya zinaa na inazorotesha utendaji kazi wa taasisi.

Masyaga amesema kutokana na madhara hayo ambayo mengi yanawakabili zaidi wasichana kuna umuhimu kwa jamii kutoa taarifa Takukuru wanapofanyiwa vitendo hivyo ili wanaohusika waweze kuchukuliwa hatua na hiyo ndio itakuwa suluhisho la kukomesha vitendo hivyo.

Amesema vitu vinavyosababisha kuwepo kwa rushwa ya ngono ni ukosefu wa maadili au mmomonyoko wa maadili kwa baadhi ya watu, tamaa na wengine tabia ya mtu mwenyewe kuendekeza masuala ya ngono.

“Leo tunapozindua dawati la jinsia katika Chuo cha Ufundi Stadi na Marekebisho kwa watu wenye ulemavu Sabasaba jambo la msingi tuhakikishe siri zinatunzwa kwa wale wanaotoa taarifa wanapofanyiwa unyanyasaji wa kijinsia na pia kuwe na wajumbe ambao wana maadili,”amesema Masyaga.

 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI