Header Ads Widget

TAARIFA ZA WAGOMBEA CCM ZAZUA SINTOFAHAMU,WAANDISHI WAKESHA UKUMBINI KUSUBIRI

 

Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media  Dodoma

Huku zikiwa zimesalia chini ya miezi mitatu kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, hamasa imekuwa kubwa katika Makao Makuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mjini Dodoma, ambako waandishi wa habari na wadau wa siasa wameendelea kusubiri kwa muda mrefu kutangazwa kwa majina ya wagombea wa chama hicho tawala.

Kwa zaidi ya saa 18 mfululizo, Ukumbi wa NEC ulioko jengo la White House  makao makuu ya CCM  umekuwa kitovu cha matarajio, sintofahamu na hali ya taharuki, baada ya kikao kilichotarajiwa kutoa majibu muhimu kuhusu wagombea kuahirishwa mara kadhaa bila ufafanuzi wa moja kwa moja kwa umma.

Awali, taarifa rasmi kutoka chama zilieleza kuwa kikao cha Kamati Kuu kilichokuwa chini ya Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, CPA Amos Makalla kingefanyika Julai 28 saa 11 jioni, lakini hakikufanyika kama ilivyopangwa. 

Saa zikayoyoma hadi usiku wa manane, huku waandishi wakipiga kambi nje ya ukumbi wakisubiri tamko la mwisho ambalo halikufika hadi alfajiri ya siku iliyofuata.

“Tumekaa hapa tangu jana jioni, kila saa tunapewa muda mpya wa kutarajia taarifa. Hadi sasa hatujapewa majibu ya uhakika,” alisema mmoja wa waandishi wa habari waliokuwa ukumbini.

Baada ya kusubiri hadi saa 10 alfajiri ya Julai 29, wanahabari walipewa maelekezo mapya kuwa mkutano huo sasa ungeendelea saa 4 asubuhi. 

Lakini hata muda huo ulipowadia, tangazo la majina ya wagombea lisingetolewa tena, na badala yake kikao kikapangwa kuendelea saa 6 mchana hali iliyoibua maswali mengi miongoni mwa wachambuzi wa siasa.

Kwa mujibu wa taarifa zisizo rasmi kutoka ndani ya chama, ucheleweshaji huo umetokana na kazi nzito ya uhakiki wa mwisho wa majina ya wagombea, inayohusisha kupitia mapendekezo ya awali kutoka vikao vya Halmashauri Kuu na Kamati Kuu ya chama.

CPA Makalla anatarajiwa kuzungumza na wanahabari mara tu kikao cha ndani kitakapohitimishwa. Taarifa hiyo inatarajiwa kuanika orodha ya wagombea wa Ubunge wa Majimbo Tanzania Bara, Viti Maalum vya wanawake pamoja na wale wa Baraza la Wawakilishi visiwani Zanzibar.

Kwa sasa, hali ya ukumbi bado ni tulivu lakini ya taharuki. Waandishi wameendelea kuripoti kila harakati zinazoendelea huku baadhi wakijipatia muda wa kupumzika kwenye magari yao, wengine wakisubiri kwa uangalifu kila dalili ya uamuzi kutoka kwa viongozi wa chama hicho.

Wadau wengi wa siasa wanaamini kuwa orodha hiyo itatoa mwelekeo mpya kwa CCM kuelekea kampeni za uchaguzi mkuu. Wananchi nao wamekuwa wakifuatilia kwa karibu kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

Pamoja na kucheleweshwa kwa taarifa hiyo muhimu, CCM imeendelea kusisitiza kuwa mchakato wa uteuzi unaongozwa na misingi ya demokrasia ya ndani ya chama, ukizingatia vigezo vya uadilifu, uwezo wa uongozi, na ushindani wa kisiasa katika maeneo mbalimbali nchini.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI