Header Ads Widget

SUA YAJA NA MITAALA YA UALIMU WA AMALI KUPUNGUZA UKOSEFU WA AJIRA KWA VIJANA


Na Farida Mangube, Morogoro

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimeanzisha mitaala mipya ya Ualimu wa Amali kwa ajili ya walimu wa shule za  sekondari, ili kuwawezesha kufundisha masomo yenye mwelekeo wa kuwaandaa wanafunzi kujiajiri. Hatua hii inalenga kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana nchini.


Akizungumza na waandishi wa habari mjini Morogoro, Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Raphael Chibunda alisema SUA imeandaa jumla ya mitaala sita ya Ualimu wa Amali, ambayo inatarajiwa kuanza kutumika rasmi kuanzia mwaka mpya wa masomo.

Mitaala hiyo inajumuisha masomo ya kilimo, ushonaji, kilimo cha mboga na bustani, lishe, pamoja na ufugaji wa viumbe  maji. Kwa mujibu wa Prof. Chibunda, masomo haya yatalenga walimu watakaoandaliwa SUA ili wakafundishe katika shule za sekondari nchini kote.


"Chuo chetu kimeamua kuanzisha mitaala hii kwa lengo la kuwajengea wanafunzi uwezo wa kujitegemea kupitia stadi mbalimbali za maisha. Tunatarajia hatua hii itachangia kupunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la ajira nchini," alisema Prof. Chibunda.


Aliongeza kuwa mitaala hiyo imeandaliwa kwa kuzingatia mahitaji ya sasa ya jamii na soko la ajira, na inatarajiwa kuleta mapinduzi chanya katika sekta ya elimu na maendeleo kwa vijana.


Hatua hii ya SUA ni sehemu ya mikakati ya taasisi za elimu ya juu nchini kuhakikisha elimu inayotolewa inawajengea vijana uwezo wa kutumia maarifa yao kwa kujiajiri na kuchangia katika maendeleo ya uchumi wa taifa.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI