Header Ads Widget

SAMATTA, MASTAA WA SIMBA NA YANGA KUNOGESHA ALLIANCE DAY MWANZA




 Na chausiku said

Matukio Daima, Mwanza


Nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta, ataongoza kikosi cha mastaa zaidi ya 18 kutoka klabu kongwe nchini Simba, Yanga na timu nyingine za Ligi Kuu katika tamasha la Alliance Day litakalofanyika Julai 9 mwaka huu kwenye Uwanja wa Nyamagana, jijini Mwanza.

Tamasha hilo limeandaliwa na Kitivo cha Michezo cha Alliance kwa lengo la kuenzi maisha ya aliyekuwa mwasisi wa kitivo hicho, marehemu James Bwire, sambamba na kusherehekea Jubilee ya miaka 25 tangu kuanzishwa kwa shule hizo za michezo.

Mchezo huo unatarajiwa kuanza saa 10 jioni, ukitanguliwa na matukio mbalimbali ikiwemo mbio za hisani zitakazowashirikisha wafanyakazi wa kituo, wadau wa michezo na mechi za watoto kutoka vituo vya kukuza vipaji vya soka jijini Mwanza.




Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Kituo cha Alliance, Stephano Nyaitati, alisema zaidi ya wachezaji 18 wamethibitisha kushiriki tamasha hilo. Miongoni mwao ni nyota wa Yanga kama Prince Dube, Israel Mwenda, Djigui Diarra, Maxi Nzengeli, Salum Abubakar 'Sure Boy' na Jonas Mkude.

"Wengine waliothibitisha ni Novatus Dismas, Mourice Abraham, Hussein Kazi, Said Ndemla, Ladack Chasambi, Yusuf Kagoma na Hassan Dilunga, ambao wote wanatarajiwa kuwasili Mwanza Julai 8," alisema Nyaitati.

Aliongeza kuwa mbali na kumuenzi Bwire, tamasha hilo pia litatoa fursa kwa kituo kupanga mikakati ya msimu mpya, ikiwemo kupandisha timu yao daraja hadi Championship na kuboresha miundombinu ya viwanja ili vikidhi vigezo vya Ligi Kuu.

"Tunalea zaidi ya vijana 200 tunaowasomesha na kuwafundisha mpira. Hawalipi chochote. Ili kituo kiendelee kuwa hai, tunahitaji msaada wa wadau kutuwezesha," alieleza.

Kwa upande wake, Mratibu wa tamasha hilo, Jackson Mwafulango, alitoa wito kwa mashabiki wa soka na wadau wa michezo kujitokeza kwa wingi kushiriki na kuchangia mafanikio ya tamasha hilo.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI