Header Ads Widget

RC MTANDA-MWANZA YAVUNA MATUNDA YA UVUVI WA KISASA

 

Na Hamida Ramadhan, MatukioDaima App Dodoma

MKUU wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, amesema mkoa wake umeendelea kunufaika kwa kiasi kikubwa na mageuzi katika sekta ya uvuvi na ufugaji wa samaki, hasa kupitia matumizi ya teknolojia ya kisasa katika uzalishaji na usindikaji wa mazao ya samaki.

Akizungumza leo Julai 16 2025 na waandishi wa habari jijini Dodoma  kuhusu mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita, Mtanda amesema idadi ya vizimba vya kufugia samaki (fish cages) imeongezeka kutoka 1,664 mwaka 2020 hadi 2,715 mwaka 2025, sawa na ongezeko la vizimba 1,051.

Katika kipindi cha mwaka 2024 pekee, amesema, zaidi ya tani 43,657.6 za minofu ya samaki zilichakatwa huku tani 81,812 zikisafirishwa nje ya nchi kupitia Uwanja wa Ndege wa Mwanza.

Aidha, usafirishaji wa mabondo ya samaki kwenda nje ya nchi umeongezeka kutoka kilo 431,721 mwaka 2020 hadi kilo 495,448 mwaka 2024 — ongezeko la kilo 63,727.

Mkuu huyo wa mkoa pia amebainisha kuwa idadi ya mabwawa ya kufugia samaki imeongezeka kutoka 286 mwaka 2020 hadi mabwawa 531 mwaka 2025, ikiwa ni ongezeko la mabwawa 245.

“Haya mafanikio ni ushahidi kuwa juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha uchumi wa buluu na sekta ya uvuvi zimezaa matunda Mapato kutokana na shughuli za uvuvi yameongezeka kutoka shilingi bilioni 4.4 mwaka 2020 hadi bilioni 8.2 mwaka 2025,” amesema Mtanda.

Amesisitiza kuwa mkoa utaendelea kuhamasisha uwekezaji, utafiti na matumizi ya teknolojia ili kuhakikisha wananchi wa Mwanza, wakiwemo wavuvi wadogo na wafanyabiashara wa dagaa, wananufaika ipasavyo na rasilimali za Ziwa Victoria.

Mwisho

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI