Na Ashrack Miraji Matukio Daima
Same — Benki ya NMB imeendelea na zoezi la kuwajengea uwezo wanafunzi wa elimu ya sekondari juu ya usimamizi wa fedha, ikiwa ni sehemu ya kampeni endelevu ya kuhamasisha matumizi salama ya huduma za kifedha miongoni mwa vijana. Zoezi hilo linafanyika sambamba na mapokezi ya wanafunzi wa kidato cha tano na sita katika shule mbalimbali za Wilaya ya Same.
Katika awamu ya hivi karibuni, timu ya maafisa kutoka Benki ya NMB ikiongozwa na Kaimu Meneja wa Tawi la NMB Same, Bw. Ibrahim Ngonwe, ilifanya ziara katika Shule ya Sekondari Kisiwani kwa ajili ya kutoa elimu ya kifedha kwa wanafunzi wapya, pamoja na kuwawezesha kufungua akaunti binafsi kwa madhumuni ya kuhifadhi fedha zao kwa usalama.
Mbali na wanafunzi, wazazi na walezi walihusishwa moja kwa moja katika mafunzo hayo, wakielekezwa njia rasmi, salama na za kisasa za kuwatumia wanafunzi fedha kwa ajili ya mahitaji yao ya kila siku shuleni. Mafunzo hayo yalilenga kupunguza utegemezi wa njia zisizo rasmi ambazo huongeza hatari ya upotevu wa fedha au matumizi yasiyopangwa.
Takwimu za awali zinaonesha kuwa jumla ya akaunti zaidi ya 400 tayari zimefunguliwa kwa wanafunzi wa shule mbili — Sekondari ya Same na Kisiwani — hatua inayoashiria mwitikio chanya kutoka kwa jamii. Zoezi hili linaendelea kutekelezwa katika shule zote zenye kidato cha tano na sita wilayani humo, huku awamu ijayo ikipangwa kuelekezwa kwa shule zenye kidato cha nne na chini (O-Level).
Kwa upande wake, Benki ya NMB imeeleza dhamira yake ya kuendelea kushirikiana na sekta ya elimu ili kuimarisha elimu ya fedha kwa vijana, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa muda mrefu wa kukuza kizazi chenye maarifa ya kifedha na uwezo wa kufanya maamuzi sahihi ya kiuchumi kuanzia ngazi ya chini.
0 Comments