Na Fadhili Abdallah,Kigoma
Mkuu wa mkoa Kigoma Balozi Simon Siro amewataka watumishi wa umma mkoani Kigoma kuanza mpango wa uwekezaji wa shughuli za uchumi na biashara wakiwa bado kazini kutokana na fursa kubwa waliyonayo badala ya kusubiri kupata mafao ya kustaafu ndiyo kuanza kutekeleza mpango huo.
Balozi Siro alisema hayo wilayani Buhigwe mkoani Kigoma akiendelea na ziara ya kiserikali mkoani humo ambapo alisema kuwa kwa sasa ambapo watumishi wa umma bado wanaendelea na utumishi wanayo nafasi ya kuweza kuanzisha biashara na shughuli za kiuchumi na kuwa rahisi kupata mikopo sambamba na usaidizi wa kitaalam kutoka kwa wataalam wenzao katika utumishi wa umma.
Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa watumishi wa umma wanapaswa kuwa kioo na kielelelezo cha mpango wa serikali wa kuvutia uwekezaji kwani wanajua mambo mengi ambayo serikali inataka kufanya hivyo wanapaswa kutumia fursa hiyo kuona maeneo wao kama watanzania wanaweza kutumia mitaji yao pamoja kuomba mikopo kuanzisha shughuli mbalimbali za uchumi na biashara.
Katika kuunga mkono hilo Mkuu huyo wa mkoa Kigoma amewataka wataalam katika halmashauri za mkoa Kigoma kutumia nafasi zao kuwasaidia wananchi kufuga kisasa,kulima kisasa kwa kufuata utaalam ili shughuli zao ziwe na tija kwao lakini pia kwa taifa.
Katika mkutano huo Afisa kilimo na mifugo wa Halmashauri ya wilaya Buhigwe, Alphonce Haule alisema kuwa halmashauri imeanza kutekeleza shughuli mbalimbali za kukuza uchumi na biashara ikiwemo kuanzia kituo ambapo imeanza kuzalisha ng’ombe na mbuzi bora ambao wananchi wanaweza kufuga na mifugo hiyo ikafugwa kibiashara.
Kwa upande wake Afisa biashara wa halmashauri hiyo, Joseph John alisema kuwa wilaya imeanzisha kituo cha biashara cha pamoja ambapo takwimu mbalimbali za shughuli za kiuchumi na biashara zinakusanywa ikiwemo tafiti maeneo ya uwekezaji, urasimishaji biashara, masoko na namna watu mbalimbali wanaweza kukutana na wafanyabiashara wengine kupeana fursa za kibiashara.
0 Comments