Kutokana na changamoto ya uelewa mdogo wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) miongoni mwa walimu na wanafunzi katika shule mbalimbali, kata ya Inyala wilaya Mbeya imeanza kupewa mafunzo ya TEHAMA ili kuongeza ujuzi na ufanisi katika ufundishaji wa masomo ya TEHAMA kwa wanafunzi.
Wakizungumza katani humo, walimu hao wamesema kuwa elimu ya TEHAMA ni msingi muhimu katika mfumo wa kisasa wa elimu, hivyo ni lazima wawe mstari wa mbele kuhakikisha wanafunzi wanapata maarifa sahihi na ya kisasa.
Wameishukuru Serikali katika kata hiyo kwa kuhakikisha wanaungana kununua kompyuta kwa ajili ya shule za sekondari katani humo hatua ambayo itasaidia kwa sehemu kubwa kuongeza kiwango cha elimu.
Kwa upande wao, baadhi ya viongozi wa elimu na waratibu wa mafunzo wamesisitiza kuwa lengo kuu ni kukuza elimu ya TEHAMA nchini, kwa kuanzia na walimu kama nguzo kuu ya utekelezaji wake.
Mwalimu Jofrey Lwanzile Afisa Elimu taaluma Halmashauri ya wilaya ya Mbeya, amesema Serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya elimu ili kuhakikisha watoto wanapata elimu bora kwa maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Mbeya ambaye pia ndiye Diwani wa kata ya Inyala Mhe. Mwalingo Kisemba amewashukuru viongozi mbalimbali katani kwake kwa kuungana kuhakikisha wananunua kompyuta 27 kwa ajili ya shule tatu za Sekondari kwenye kata hiyo ambapo pamoja na kusimamia miradi mbalimbali ya kimaendeleo Diwani huyo amekuwa na mzigo mkubwa wa kuinua sekta ya elimu.
Elimu ya TEHAMA na teknolojia kwa ujumla ni chachu muhimu ya maendeleo ya elimu kwa ujumla na hivyo wanafunzi wanahimizwa kuwa makini na kushiriki kikamilifu katika masomo hayo.
0 Comments