Header Ads Widget

WAJAWAZITO WASHIRIKI MBIO ZA UTALII KANDA YA ZIWA.

 


Na Chausiku Said

Matukio Daima Mwanza

Zaidi ya wanawake 100 wakiwemo wajawazito wameungana na wanariadha katika Mbio za kiutalii Kanda ya Ziwa 2025, kwa  kutembea umbali wa km 2.5 kwa lengo la kuhamasisha afya ya mama na mtoto, huku washindi wakijinyakulia zawadi ya fedha katika mashindano hayo.

Mbio hizo za Lake zone International Tourism Marathon 2025 zilizofanyika leo juni 29 katika viwanja vya Nyamagana Jijini Mwanza yenye lengo la kutembelea na kutangaza vivutio vya utalii ili kukuza uchumi wa Kanda ya Ziwa pamoja na kumsadia mjamzito kuimalisha mfumo mzima na kupata Mtoto aliye salama, na uzazi salama na kutengeneza Taifa lililosalama.

Akizungumza baada ya mashindano, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dkt. Jesca Lebba, alisema“Mazoezi ni tiba. Mama mjamzito anayefanya mazoezi hupunguza hatari ya upasuaji, uchovu wa uzazi na huongeza uwezekano wa kujifungua salama.”

Dkt. Lebba alisema serikali inashukuru wadau wa michezo na afya kwa kuandaa tukio hilo ambalo linakwenda sambamba na mkakati wa taifa wa kupunguza vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua.

Alisema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan,kupitia filamu ya Royal Tour imeongeza watalii wanaokuja kutembelea vivutio vilivyopo nchini ikiwemo Kanda ya Ziwa.

“Niwapongeze Kilimanjaro One Sports Promotion na wadau wa michezo kwa kusimamia jambo hili kwa ufanisi kwa kuangazia ngazi ya chini,hivyo naamini tutaendelea kuyafanya haya kwa kuwa afya ni mtaji wa binadamu,”alisema Dr.Lebba.



Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kilimanjaro One Sports Promotion Ltd,Mohamed Khatibu,alisema mbio hizo zimeanzishwa kwa mara ya kwanza Kanda ya Ziwa zimebebwa na wajawazito ambao ndio walengwa wakuu.

“Tuliangalia kusaidia jamii katika eneo muhimu la afya hasa wajawazito na watoto,kulikuwa na malalamiko ya uhaba a vifaa vya uzazi kwa wajawazito na uvivu wa kutofanya mazoezi,Lake Zone Tourism Marathon inalenga vifaa vya uzazi vitakavyogawiwa katika vituo vya kutolea huduma ili kuunga mkono afya ya mama na mtoto hasa wajawazito,”alisema.

Khatibu alisema baada ya kufanikiwa Kanda ya Ziwa,watakaa chini na kufikiria jinsi ya kuendelea kuwasaidia akinamama ama wataongeza eneo jingine kwa sababu bado kuna mahitaji kwa akinamama wajawazito.

Baadhi ya wajawazito walioshiriki mbio hizo Pracidia Philimon na Marina Mathias,waliipongeza Kilimanjaro One Sports Promotion kwa maono hayo,yatasaidia kupunguza upasuaji kwa baadhi ya wajawazito wakati wa kujifungua.


“Wamefanya kazi nzuri,kufanya mazoezi kunasaidia nyonga kuwa sawa,bila mazoezi zinauma kwa sababu wajawazito wengi tu wavivu,tunatumia muda mwingi kulala badala ya kutembea walau hata km 1 hadi 2,”alisema Pracidia.

Kwa upande wake Marina ameeleza kuwa “Kilimanjaro One Sports wametuheshimisha, mazoezi ni fursa yanasaidia kufungua nyonga na kumfanya mtu kuwa mchangamfu, sasa visu tutaviepuka maana tulikuwa tunateswa na uvivu,”alisema na kuongeza kuwa mbio hizo zikifanyika kila mara upasuaji kwa wajawazito utapungua.

Aidha,John Joseph aliyeshika nafasi ya kwanza kwa wanaume mbio za km 21,aliwapongeza wajawazito walioshiriki mbio hizo na kuwataka waendelee kuwatia moyo wajawazito wengine kuzingatia mazoezi.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI