NA CHAUSIKU SAID
MATUKIO DAIMA MWANZA.
Ushirikishwaji wa Watanzania katika sekta ya madini umeelezwa kuwa chachu muhimu katika kuchochea uchumi wa Tanzania na kuongeza pato la taifa, huku ikiimarisha ajira, ujuzi na ukuaji wa viwanda vya ndani.
Akizungumza katika kufunga kongamano la nne la jukwaa la ushirikishwaji wa Watanzania katika sekta ya madini leo juni 18 Mwaka huu Mkurugenzi wa Sera na Mipango kutoka Wizara ya Madini, Augustine Ollal, kwa niaba ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, amesema kuwa ushirikishwaji huu si tu kwamba unaongeza mapato ya serikali, bali pia unawanufaisha moja kwa moja wananchi.
“Kwa sasa asilimia 99 ya waajiriwa katika sekta ya madini ni Watanzania. Hii ina maana kwamba fedha wanazolipwa kama mishahara zinabaki ndani ya nchi na kuzunguka kwenye uchumi wetu,” alisema Ollal. “Zaidi ya ajira, Watanzania pia wanapata ujuzi na uzoefu ambao kwa mazingira ya kawaida wasingeweza kuupata kama makampuni haya yasingekuwepo.”
Aidha, Ollal ameimiza Watanzania kuchangamkia fursa zilizopo hasa kwa kuwekeza kwenye viwanda vinavyotengeneza bidhaa zinazotumika katika migodi, akibainisha kuwa soko la bidhaa hizo lipo na linaendelea kukua kutokana na matakwa ya kanuni za ushirikishwaji.
“Kama wazalishaji wataongeza ubora wa bidhaa zao, si tu kwamba zitasambazwa ndani ya nchi, bali pia tutafungua masoko ya kimataifa,” aliongeza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Biashara ya Madini kutoka Tume ya Madini, Venance Kasiki, alisisitiza umuhimu wa taasisi za kifedha kutoa mikopo kwa watoa huduma wa ndani ili kuwawezesha kushindana kwa usawa na wawekezaji wa nje.
“Tume ya Madini itawasiliana na sekta za kibenki kuona namna wanavyoweza kuunga mkono watoa huduma na wasambazaji wa ndani kwa kuwapa mikopo nafuu itakayowawezesha kuongeza uwezo wao wa kushindana,” alisema Kasiki.
Kamishna wa Tume ya Madini, Mhandisi Theonestina Mwasha, alisisitiza kuwa makampuni ya uchimbaji, wasambazaji na watoa huduma wana wajibu wa kutekeleza matakwa ya ushirikishwaji wa Watanzania kwa hiari ili matokeo chanya yaendelee kuonekana.
Kwa ujumla, kongamano hilo limeonyesha kuwa ushirikishwaji wa Watanzania katika sekta ya madini ni nyenzo muhimu ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii, ikiwa serikali na sekta binafsi zitaendelea kushirikiana katika kuhakikisha fursa zilizopo zinawanufaisha Watanzania wengi zaidi.
0 Comments