Na Moses Ng'wat, Mbozi.
Hatimaye ndoto ya wananchi wa Mkoa wa Songwe, hususan wa Wilaya za Mbozi na Momba, ya kuona barabara ya Kamsamba - Mlowo yenye urefu wa Kilometa 130.2 inajengwa kwa kiwango cha lami inaanza kutimia, baada ya Serikali kusaini mikataba miwili ya kuanza ujenzi wa sehemu ya barabara hiyo.
Mikataba hiyo, iliyosainiwa Juni 22, 2025 kati ya serikali kupitia Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) na Mkandarasi M/s Classik (T) Ltd kutoka Dar es Salaam na kushuhudiwa na Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Gidfrey Kasekenya na Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo na viongozi mbalimbali wa serikali na kisiasa.
Akitoa maelezo kabla ya mikataba hiyo kusainiwa, Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Mhandisi Mohamed Besta alisema mikataba hiyo inalenga ujenzi wa jumla ya kilometa 10 za lami ambapo kilometa 5 zikitoka Mlowo katika Wilaya ya Mbozi kuelekea Kamsamba, Wilayani Momba na kilometa 5 nyingine kutoka Kamsamba kuelekea Mlowo, huku kila mkataba ukigharimu Shilingi bilioni 8.5.
Mhandisi Besta amesema hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa awamu ya kwanza ya ujenzi wa barabara hiyo muhimu kiuchumi na kijamii, inayopitia kata tajiri za kilimo kama Ntungwa, Utambalila, Nambizo, Itaka, Halungu na Igamba.
Alisema barabara hiyo pia inaunganisha mikoa mitatu ya Songwe, Katavi na Rukwa.
Kwa mujibu wa Mhandisi Besta, tayari upembuzi yakinifu na usanifu wa barabara nzima kutoka Kamsamba hadi Mlowo (km 130.2) pamoja na mchepuo wa Utambalila - Chitete (km 17) umekamilika tangu mwaka 2020, na maandalizi ya miundombinu kama madaraja na mabox kalavati yanaendelea kujengwa.
“Hii ni hatua kubwa inayothibitisha dhamira ya Serikali chini Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ya kuunganisha maeneo ya uzalishaji na masoko ” Alisema Mhandisi Besta.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Chongolo, akizungumzia umuhimu wa barabara hiyo alisema ni barabara ya uchumi kwa usafirishaji wa mazao ya kilimo na kuyafikia masoko, hususani zao la mpunga unaozalishwa kwa wingi katika bonde la Kamsamba.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Songwe, Ranwell Mwampashi, alisema kuanza kwa ujenzi huo ni matokeo ya utekelezaji wa Ilani ya chama hicho.
Nao wabunge, George Mwanisongole (Mbozi) na Kondesta Sichalwe (Momba) wakizunhhumza kwa nyakati tofauti baada ya mikataba hiyo kusainiwa katika Wilaya zao hawakusita kuonesha fuuraha zao na kuishukuru serikali, huku wakianisha kuwa kulamilika kwa ujenzi wa barabara hiyo kutachochea maendeleo ambapo muda wa kusafiri utapingua kutoka saa nane hadi kuwa chini ya saa tano, ikiwemo kupungua kwa gharama za nauli.
Wananchi wa Mlowo na Kamsamba wameipokea taarifa hiyo kwa furaha, wakisema barabara hiyo itafungua fursa zaidi za kibiashara na kupunguza changamoto za usafiri, hususan vipindi vya mvua.
Mwisho.
0 Comments