Na Shomari Binda-Musoma
MBUNGE wa Viti maalum mkoa wa Mara Ghati Chomete amempongeza mkuu wa mkoa wa Mara Kanali Evans Mtambi kwa kuandaa kongamano la maonyesho ya madini mkoa wa Mara.
Akizungumza na Matukio Daima leo juni 8,2025 amesema maonyesho hayo ambayo yamefanyika kwa mara ya kwanza mkoani Mara yamekuwa na ubora wa hali ya juu na yameutangaza vyema na kuupaisha mkoa.
Amesema kwa mwana Mara na Mtanzania yetote ambaye amefuatilia kwa karibu maonesho ya madini yaliyofanyika mkoani Mara kuanzia tarehe 3 hadi 6 juni,2025 atakuwa ameridhishwa na ubunifu huo uliofanywa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara chini ya Mkuu wa Mkoa Kanali Evans Alfred Mtambi.
Mbunge huyo amesema maonesho hayo ambayo yalilenga kutambua fursa mbalimbali za madini katika mkoa wa Mara, kusikiliza kero na changamoto za wachimbaji na kuzipatia ufumbuzi pamoja na kuhamasisha wana Mara na Watanzania kwa ujumla kuchangamkia fursa za madini hususani katika mkoa wa Mara.
Amesema maonesho hayo pia yamechangia kuongezeka kwa mzunguko wa kibiashara kwa watu wa mkoa wa Mara hususani Manispaa ya Musoma wakiokuwa wenyeji wa maonesho hayo.
Ameongeza kuwa makundi mbalimbali ya wajasiriamali, bodaboda, wafanyabiashara na watu wenye mahoteli wamenufaika kwa namna moja au nyingine kupitia maonyesho hayo.
"Ni ubunifu wa kipekee na ambao umemtambulisha kwa namna ya kipekee Kanali Evans Alfred Mtambi Mkuu wa Mkoa wa Mara kwa namna alivyokusudia kuupeleka mbele kimaendeleo mkoa wa Mara.
"Wito wetu kama wana Mara ni angalau maonesho haya yafanyike kila baada ya miezi sita (6) kwa kufanya mzunguko kwenye Halmashauri za Wilaya katika Mkoa wa Mara.
Mbunge Ghati ameipongeza pia Ofisi ya Mkuu wa Mkoa pamoja na Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mara n̈ wadau wa madini ikiwemo Wizara kwa kumpa ushirikiano mkuu huyo wa mkoa na kufanikisha maonyesho hayo.
0 Comments