Header Ads Widget

MAMBO 6 MUHIMU YA KUKUMBUKWA YA BUNGE LA 12 LA TANZANIA

Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linavunjwa rasmi leo Juni 27, 2025 na Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye pia anatarajiwa kulitunuku hotuba ya mwisho.

Moja ya mafanikio makubwa ya bunge hili ni kuulizwa kwa maswali zaidi ya 20,300, kupitishwa kwa miswada 58, maazimio 922 na mikataba 12 ya kimataifa, likiwemo azimio la pongezi kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake wa mfano.

Bunge hili lilianza rasmi Novemba 1, 2020, likifunguliwa na aliyekuwa Rais wa awamu ya tano, hayati John Pombe Magufuli. Kuvunjwa kwa bunge hili kunafungua njia rasmi ya kuanza kwa mchakato wa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

Kama ilivyo kwa mabunge yaliyotangulia, Bunge la 12 pia limeacha historia yake ya kipekee, likiwa na matukio ya kisiasa, kisheria na kijamii ambayo yataendelea kukumbukwa kwa muda mrefu.

Haya hapa ni mambo makuu sita yaliyolitambulisha Bunge la 12 katika historia ya mabunge Tanzania

1. Bunge la Maspika wawili

Job Ndugai, aliyekuwa Spika wa sita wa Bunge, alijiuzulu Januari 2022 na kumpisha naibu wake Dkt. Tulia Ackson

Bunge hili litakumbukwa kwa kuwa na maspika wawili tofauti katika kipindi chake: Job Ndugai na Dkt. Tulia Ackson. Job Ndugai, aliyekuwa Spika wa sita wa Bunge, alijiuzulu Januari 6, 2022, baada ya kukosoa hadharani hatua ya serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kukopa fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Kauli yake maarufu kwamba "kuna siku nchi itakuja kupigwa mnada" ilizua mjadala mkali wa kisiasa. Ambapo akizungumza katika shughuli ya kimila mjini Dodoma, Ndugai alisema:

"Juzi mama ameenda kukopa trilioni 1.3 na tuna majengo ya madarasa na vituo vya afya ambavyo vinajengwa kwa tozo, kipi bora sisi tubanane hapa tujenge wenyewe bila madeni makubwa yasiyoeleweka."

Rais Samia hakukaa kimya. Alimjibu kwa kauli iliyotafsiriwa kuwa ya moja kwa moja dhidi ya Ndugai:

"Mtu na akili yake anasimama na anahoji kuhusu mikopo na tozo, sio lolote ni homa ya 2025, kwa mtu ambaye nilimtegemea kushirikiana naye kwenye maendeleo, sikutegemea kama angesimama na kusema maneno hayo."

Ingawa Ndugai hajawahi kutangaza rasmi nia ya kugombea nafasi ya juu zaidi nchini, alikana kukashifu serikali na alikuwa muungwana na kuomba radhi alipozungumza na vyombo vya habari "nitumie fursa hii kupitia kwenu kumuomba radhi sana mheshimiwa rais na kwa watanzania wote". Baada ya kujiuzulu kwake, Dkt. Tulia Ackson aliyekuwa Naibu Spika, alichaguliwa kuwa Spika wa 7 wa Tanzania kwa kura zote 376 zilizopigwa (100%), tukio la kipekee katika historia ya mabunge ya Tanzania.

2. Mvutano wa ubunge wa Halima Mdee na wenzake 18.


Bunge la 12 pia liligubikwa na mvutano wa muda mrefu kuhusu uhalali wa ubunge wa Halima Mdee na wabunge wengine 18 wa viti maalum kutoka CHADEMA waliofukuzwa uanachama na kamati kuu ya chama hicho Novemba 2020.

Licha ya kufukuzwa kwao, Bunge la 12 liliendelea kuwatambua kama wabunge halali, jambo lililozua sintofahamu ya kisheria na kisiasa.

Uwepo wa mbunge wakiwemo wa viti maalumu unabebwa na baraka za kisheria kutoka kwa chama chake. Kwa mujibu wa sheria anapofukuzwa uanachama, na ubunge wake unakoma. Wabunge hawa 19 waliendelea kuhudhuria vikao vya bunge la 12 hadi mwisho wa muhula wa bunge.

Tukio hili limeendelea kuwa rejea katika mijadala kuhusu mipaka ya mamlaka ya vyama vya siasa dhidi ya mihimili mingine ya dola, hususani Bunge, pamoja na tafsiri na utekelezaji sheria kwa vyama vya siasa na mamlaka zingine.

3. Bunge na mjadala wa utekaji uliokosa nafasi rasmi?


Spika wa bunge la 12 Tulia Ackson aliyepokea kijiti kutoka kwa Job Ndugai
Kwa kipindi kirefu, taarifa kuhusu matukio ya utekaji na watu kupotea zimekuwa zikiripotiwa kupitia vyombo vya habari na mitandaoni, huku Jeshi la Polisi likitajwa kuhusika. Mbunge wa Kawe (CCM), Josephat Gwajima, alidai kufanya utafiti binafsi na kubaini kuwa watu takribani 83 wametekwa katika miaka ya karibuni.

Wengi walimkosoa kwa kutowasilisha hoja hiyo rasmi bungeni licha ya kuwa mbunge. Hata hivyo, wapo waliomtetea wakidai hoja hiyo haikupewa nafasi bungeni. Mbunge wa Nkasi Kaskazini (CHADEMA), Aida Khenani, pamoja na mbunge wa viti maalumu, Anatropia Theonest, waliwahi kuligusia suala hilo mwaka 2024.

Mwaka 2025, Jesca Msambatavangu, mbunge wa Iringa Mjini kupitia CCM, alilihoji bungeni, lakini Spika Tulia Ackson alimwelekeza:

"Mheshimiwa Msambatavangu leta kama swali la msingi ili serikali iweze kujibu kikamilifu."

Alipoulizwa na Wasafi Media, chombo cha habari Tanzania, kuhusu kutekwa kwa watu na Bunge kutojadili hoja hiyo, mbali na kusema neno kutekwa linatumiwa kwa mazoea bila ushahidi, Spika Tulia alisema:

"Kanuni yetu inaruhusu jambo la dharura, yule anayetoa hoja ya dharura ni lazima liwe jambo ambalo Bunge tukishajadili, tunaazimia, tunaiagiza serikali cha kufanya... Hii hoja ya utekaji, unapoleta bungeni, kile tunachoazimia ni maelekezo ya serikali. Ukisema kwamba polisi wanateka watu, sawa, unataka Bunge lijadili? Wewe unao ushahidi? Huna wa kwamba ni Polisi wanaoteka?"

Jeshi la Polisi kupitia msemaji wake David Misime lilikanusha kuhusika na utekaji wowote, huku serikali ikisisitiza msimamo huo.

Mbali na watu kujiteka, Misime alito sababu za kupotea kwa watu kuwa ni "wivu wa mapenzi, imani za kishirikina, kugombea mali, kulipiza kisasi, kwenda nchi nyingine kujifunza misimamo mikali, na kukimbia mkono wa sheria baada ya kufanya uhalifu."

4. Bunge lisilokuwa na kambi rasmi ya upinzani


Aida Kenani, mbunge wa Nkasi Kaskazini, mbunge pekee wa kuchaguliwa wa chama kikuu cha upinzani CHADEMA

Bunge la 12 lilikuwa na upinzani mdogo zaidi kuwahi kushuhudiwa tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992. Kati ya wabunge 264 wa kuchaguliwa, ni 8 tu waliotoka nje ya CCM. ACT wabunge -4, CUF-3 na Chadema 1. Kwa ujumla, karibu asilimia 97 ya wabunge walikuwa ni wa CCM, huku vyama vya upinzani vikiwa na idadi ndogo ya wabunge isiyotosha kuunda kambi rasmi ya upinzani bungeni.

Kutokana na idadi hiyo ndogo, hakukuwa na kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani bungeni wala baraza kivuli la mawaziri. Dk. Marcosy Albanie, mchambuzi wa siasa, aliwahi kusema:

"Wabunge wa upinzani ndiyo waliokua wanawasaidia wabunge wa CCM kuamka na kujikuta wakitekeleza wajibu kama wabunge... kwa sasa jambo hili haliwezi kutokea."

Naye Spika wa zamani, Job Ndugai, aliwahi kugusia hali hiyo akisema:

"Ni kweli kabisa kwamba wabunge wengi wa Bunge la 12 wanatoka CCM, lakini hiyo haimaanishi kwamba litakuwa Bunge la ndiyo ndiyo ndiyo… wala hapana hapana hapana."

Mbunge wa Jimbo la Kisesa, Luhaga Mpina anathibitisha hili kwani ndiye mbunge aliyechomoza zaidi miongoni mwa wabunge wa CCM kujadili hoja kinzani dhidi ya Serikali.

5. Je, lilikuwa Bunge lilipooza?


Waheshimiwa Mawaziri na Manaibu Waziri wakitoa ufafanuzi kuhusu Hoja zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge wakati wa mjadala wa Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2024 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026.

Wapo wanaoamini kuwa Bunge la 12 halikuwa na mvuto wala msisimko wa kisiasa kama mabunge yaliyotangulia, hususan lile la tisa chini ya Spika Samuel Sitta (2005–2010) lililojulikana kwa kauli mbiu ya "Bunge la viwango na kasi" na hata lile la 10 na 11 lililoongozwa na spika wa kwanza mwanamke Tanzania, Anne Makinda

Kwa mfano, Bunge la tisa la Spika Sitta, liliweza kuibua mijadala mizito kuhusu kashfa ya Richmond (2008) lililomuondoa Waziri Mkuu wa wakati huo, hayati Edward Lowassa na ile ya Escrow (2014), ambazo zilisababisha mawaziri na viongozi kadhaa wakuu kujiuzulu.

Lakini Bunge la 12 lilionekana kukosa sauti mbadala kutokana na upungufu wa wabunge wa upinzani. Mijadala mingi haikuwa na changamoto ya upande mwingine, jambo lililopunguza msisimko na ufuatiliaji wa umma.

Na kwa sababu ilikuwa na wabunge wengi wa chama kimoja na wenye mtizamo mmoja kwa wengi wao, ilikuwa rahisi mijadala na hoja kupita kwa kishindo.

Mfano wa hivi karibuni ni upigaji kura wa kupitisha Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka 2025/26. Kati ya kura 378, kura 373 zilikuwa za "Ndiyo" (sawa na 98.7%), hakuna kura hata moja ya "Hapana", jambo lililoibua maoni kuwa matokeo yalikuwa yanajulikana hata kabla ya mjadala kuanza.

Usingeliona kwa mabunge yaliyopita hasa la 9,10 na 11 yaliyokuwa na nguvu kubwa ya wapinzani. Mfano mwaka wa fedha 2017/18 bajeti kuu ya serikali iligubikwa na mjadala mzito na hatimaye kupitishwa kwa kura za ndio 260 na hapana 65. Bajeti ya 2019/2020 ilipata kura za hapana 83.

6. Mijadala ya kukumbukwa na michango tata


Waziri wa Kilimo Hussein Bashe, moja ya Mawaziri walioonyesha uwezo mkubwa na ushawishi wa hoja katika bunge la 12

Licha ya changamoto, kukosa upinzani lakini Bunge la 12 halikukosa mijadala na michango ya kuvutia ikiwemo michango yenye utata:

Michango tata: Mbunge wa Kinondoni, Abbas Tarimba alipendekeza wabunge wapate namba maalum za magari; Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Musukuma aliomba wake wa wabunge watambuliwe kama VIP hasa katika sehemu zilizotengwa kwa watu mashuhuri (VIP); Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mjini Magharibi Tauhida Gallos yeye alitumia neno "kenge" dhidi ya wanaharakati, kauli iliyozua mjadala mkali.

Tozo za miamala ya simu: Mjadala huu uliwaweka wabunge kwenye presha kubwa kutoka kwa wananchi, na serikali ililazimika kufanya marekebisho. Moja ya mijadala iliyopongezwa na wananchi.

Sakata la sukari: Vuta nikuvute kati ya Luaga Mpina na Waziri wa Kilimo Hussein Bashe kuhusu vibali vya sukari ilisababisha Mpina kufukuzwa bungeni.

Mapenzi ya jinsia moja: Bunge lilipinga waziwazi azimio la Bunge la Ulaya lililotaka Tanzania kuruhusu mahusiano ya jinsia moja, jambo lililoibua mjadala mkubwa.

Ripoti za CAG: Ziliibua hoja juu ya matumizi ya fedha za umma, lakini hazikufikia uzito wa miaka ya nyuma.

Mkataba wa bandari (DP World): Bunge la 12 lilipitisha azimio kuhusu pendekezo la kuridhiwa kwa mkataba baina ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai kwa lengo la kuanzisha ushirikiano katika uendelezaji wa maeneo ya bandari nchini. Pendekezo la kampuni ya DP World ya Dubai kuendesha bandari lilizua mjadala mkubwa wa kitaifa, likipata upinzani mkali kutoka kwa wananchi na baadhi ya wanasiasa.

Sheria mpya za uchaguzi: Bunge hili pia lilipitisha sheria muhimu kama muswada wa Tume Huru ya Uchaguzi, sheria mpya ya uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani, pamoja na marekebisho ya sheria ya vyama vya siasa.

Kwa ujumla, Bunge la 12 limeacha alama zake nzuri kadhaa na zenye changamoto. Linapovunjwa rasmi, Watanzania wanabaki na kumbukumbu ya bunge la kipekee katika historia ya siasa za nchi. Matarajio sasa yanaelekezwa kwenye uchaguzi wa Oktoba na Bunge la 13, kuona kama litarejesha uhai wa mijadala na uwajibikaji kwa maslahi ya taifa.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI