Na. Matukio Daima App, Dar
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana, amesema maandalizi ya Tuzo za Utalii Duniani (World Travel Awards) yamefikia hatua nzuri na Tanzania iko tayari kuwa mwenyeji wa tukio hilo kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwake mwaka 1993 nchini Uingereza.
Akizungumza jijini Dar es Salaam baada ya kupokea taarifa ya maandalizi kutoka kwa kamati maalum ya maandalizi, Waziri Chana amelekeza kamati hiyo kuendelea kusimamia kikamilifu kila hatua ya maandalizi ili kuhakikisha hafla hiyo ya kimataifa inafanyika kwa mafanikio makubwa.
“Tunajivunia kuwa wenyeji wa Tuzo hizi kwa mara ya kwanza. Ni nafasi muhimu ya kuitangaza Tanzania kimataifa kama moja ya nchi bora katika sekta ya utalii,” amesema Waziri Chana.
Hafla hiyo ya kihistoria inatarajiwa kufanyika tarehe 28 Juni, 2025 katika Hoteli ya Johari Rotana, Dar es Salaam, na kuhudhuriwa na zaidi ya wageni 500 kutoka mataifa mbalimbali duniani.
Tuzo za Utalii Duniani ni miongoni mwa matukio ya heshima yanayotambua mafanikio ya wadau mbalimbali katika sekta ya utalii duniani kote, na mwaka huu, Tanzania imepata fursa ya kuonesha vivutio vyake adhimu na huduma bora kwa wageni wa kimataifa.
0 Comments