Na Fadhili Abdallah,Kigoma
VIONGOZI na waumini wa madhehebu mbalimbali ya kikristo katika wilaya ya Kigoma wameungana kufanya maombi ya kuliombea taifa Amani na kuuombea uchaguzi mkuu wa Rais,Wabunge na madiwani uweze kufanyika kwa Amani na salama.
Maombi hayo yaliyofanyika Katika kanisa la Anglikana Parish ya Katubuka yaliongozwa na Mchungaji wa kanisa la TAG Katubuka, Mchungaji Gaudence Jumanne yakifanyika chini ya Mwamvuli wa Kigoma Huduma kwa Yesu inayoshirikisha makanisa mbalimbali .
Akitoa maelezo kuhusu kongamano hilo la kuombea Amani Mratibu wa Huduma kwa Yesu Kigoma, Chrizostom Ruhulugu alisema kuwa maombi hayo yanakuja wakati huu mchakato wa uchaguzi Mkuu ukianza ukilenga kuunganisha Watanzania wote kushiriki harakati za uchaguzi bila vurugu wala uvunjifu wowote wa Amani.
Katika maombezi hayo Mratibu huyo Alisema kuwa pamoja na masuala ya uchaguzi Mkuu lakini pia wanaiombea nchi na viongozi wake waweze kuwa na afya njemana kuweza kutimiza wajibu wao katika kuliletea Taifa Maendeleo na ustawi bora wa wananchi wake.
Akizungumza katika kongamano hilo Mkuu wa wilaya Kigoma,Dk.Rashid Chuachua ameyataka madhehebu ya dini wilayani humo kutumia nyumba zao za ibada kuhimiza Amani na usalama kwa waumini wake na kuepuka vurugu hasa wakati huu ambapo nchi inaendelea kwenye uchaguzi mkuu.
Katika hotuba iliyotolewa kwa niaba yake na Afisa Tarafa wa Kigoma Kaskazini, Maximilian Ngasa Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa Tanzania ni kisiwa cha Amani na imekuwa kimbilio kwa nchi mbalimbali zinazotuzunguka hivyo kupotea kwa Amani katika nchi yetu italeta taabu kubwa kwa viongozi na wananchi wake maana hawana pa kwenda kwani nchi zote zinazotuzunguka zina vita kila siku.
Pamoja na hilo Dk.Chuachua aliwahimiza viongozi na waumini hao wa madhehebu ya kikristo kupigia kelele suala la ukatili wa aina mbalimbali kwenye majumbani yao kwni kwa sasa bado tatizo hilo linaendelea licha ya serikali kutekeleza mikakati mbalimbali ya kukabiliana na hali hiyo.
Mwisho.
0 Comments